Na Janeth Raphael- MichuziTv -Dodoma.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando maarufu kama Baba Levo, ameibua wasiwasi kuhusu kuendelea kwa migogoro ya ardhi nchini, akisema suala hilo limekuwa chanzo kikubwa cha migongano katika jamii kutokana na umuhimu mkubwa wa ardhi katika maisha ya watu.
Akizungumza bungeni, mbunge huyo amesema duniani kuna mambo matatu ambayo watu hupambana nayo kwa nguvu zote ambayo ni fedha, mapenzi na ardhi, akisisitiza kuwa migogoro mingi inayojitokeza nchini inahusishwa moja kwa moja na matumizi ya ardhi pamoja na mabadiliko ya matumizi ya maeneo yaliyotengwa kwa matumizi ya umma.
Mbunge huyo alihoji ni lini Serikali itaweka sheria kali zaidi zitakazodhibiti tabia ya kubadilisha matumizi ya maeneo ya wazi pamoja na maeneo yaliyotengwa kwa huduma za jamii, hali ambayo imekuwa ikichochea migogoro ya mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini.
“Ardhi imekuwa chanzo kikubwa cha migogoro. Tunaona maeneo ya wazi na yale yaliyotengwa kwa matumizi ya umma yakibadilishwa matumizi kila mara. Serikali ina mpango gani wa kuweka sheria kali kudhibiti hali hii?” alihoji Baba Levo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua dhidi ya wote wanaovamia maeneo ya wazi au kuendeleza shughuli za ujenzi bila kufuata sheria, taratibu na mipango ya matumizi ya ardhi iliyowekwa.
Mmuya ametoa onyo kali kwa wananchi wanaojihusisha na ujenzi katika maeneo yaliyotengwa kwa matumizi ya umma bila kibali halali, akisema Serikali haitasita kubomoa majengo yote yaliyojengwa kinyume cha sheria bila kujali gharama zilizotumika katika ujenzi huo.
Alisisitiza kuwa ulinzi wa maeneo ya wazi ni muhimu kwa maendeleo ya miji na ustawi wa jamii, hivyo wananchi wanapaswa kufuata sheria za mipango miji na matumizi bora ya ardhi ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.
Aidha, Serikali imewahimiza wananchi kuhakikisha wanapata vibali na kufuata utaratibu sahihi kabla ya kuanza maendeleo yoyote ya ujenzi ili kulinda maeneo yaliyotengwa kwa manufaa ya umma pamoja na kudumisha utaratibu wa mipango miji nchini.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...