*Makonda Aainisha Vipaumbele AFCON 2027 na Ajira za Vijana
Na Mwandishi wetu
BUNGE limeidhinisha bajeti ya Shilingi bilioni 525.3 kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Huku fedha hizo zikilenga kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya habari, kukuza ajira kwa vijana na kuharakisha maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027.
Akiwasilisha na kufafanua mwelekeo wa Wizara hiyo Paul Makonda alisema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 39.07 zimetengwa kwa mishahara, bilioni 28.06 kwa matumizi mengineyo, na Sh 458.19 kwa miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa Serikali imeweka mkazo mkubwa kwenye uwekezaji wa kimkakati.
Alisema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, Wizara kupitia Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali imeendelea kuimarisha mawasiliano ya umma kwa kuandaa mikutano 22 ya Msemaji Mkuu wa Serikali na vyombo vya habari, mikutano 30 ya taasisi za Serikali pamoja na mikutano 15 ya Mawaziri waliowasilisha utekelezaji wa majukumu yao na ahadi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika siku 100 za muhula wa pili.
“Lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, kwa wakati na kwa uwazi kuhusu utekelezaji wa shughuli za Serikali,” alisema Makonda.
Aidha, Wizara imechapisha nakala 20,000 za jarida la Nchi Yetu linaloelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Makonda alisema Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) linaendelea kupanua usikivu kwa kujenga vituo vya redio vya FM katika wilaya 18 na kupokea mitambo kwa wilaya nyingine tano, huku miradi mingine ikitekelezwa kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).
Alisema pia TBC imeboresha maudhui kwa vijana kupitia majukwaa ya Bongo FM, TBC2 na TBC Mtandao, huku chaneli ya Tanzania Safari ikiendelea kuitangaza Tanzania kimataifa kwa kurusha vipindi 1,125 katika lugha tano.
Kwa mujibu wa Makonda, Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) imeanzisha maktaba ya kidijiti yenye zaidi ya matoleo 12,600 ya magazeti, picha 2,499 na makala 2,100, pamoja na kuandaa makala 2,973 za kimkakati.
Aidha, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imesajili waandishi 4,139, ambapo 3,357 wamepatiwa ithibati, huku malalamiko 14 ya ukiukwaji wa maadili yakishughulikiwa.
Makonda alisema Serikali imetenga Shilingi bilioni 20 kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa kwa ajili ya kuwawezesha vijana, ambapo tayari Shilingi bilioni 2 zimetolewa kwa mikopo ya watengeneza maudhui mtandaoni.
Zaidi ya vijana 931 wamepata mafunzo ya kuboresha ubora wa kazi zao, wengi wao wakiwa wanawake.
Kiswahili chaimarika kimataifa
Alisema Wizara kupitia BAKITA imekusanya maneno milioni 61 katika Kongoo ya Kiswahili ya Taifa (KOKITA), ikiwa ni juhudi za kuifanya lugha hiyo iendane na teknolojia ya kisasa ikiwemo akili unde (AI).
Aidha, Kiswahili kimepata hadhi ya kuwa lugha rasmi ya mikutano ya UNESCO, hatua iliyotajwa kuwa ya kihistoria kwa bara la Afrika.
Kuhusu michezo, Makonda alisema Serikali imeongeza kasi ya maandalizi ya AFCON 2027, ambapo ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa umefikia asilimia 95 na ujenzi wa Uwanja wa Arusha asilimia 77.5.
Aliongeza kuwa Tanzania tayari imelipa dola milioni 30 kama ada ya uandaaji wa mashindano hayo, akisisitiza kuwa tukio hilo litafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi.
Makonda alisema Serikali imewasilisha andiko la vazi la kanga UNESCO ili litambuliwe kama urithi wa utamaduni wa dunia, huku zaidi ya Shilingi bilioni 3.5 zikitolewa kwa miradi 229 ya sanaa.
Aliongeza kuwa juhudi za kulinda maadili zimeimarishwa kupitia mkakati wa taifa pamoja na vipindi maalum vya kuelimisha umma.
Kwa ujumla, alisema bajeti hiyo inalenga kuleta mageuzi makubwa katika sekta za habari, utamaduni, sanaa na michezo, huku Serikali ikijiandaa kutumia kikamilifu fursa za matukio ya kimataifa kama AFCON 2027 na Miss World 2027 kuitangaza Tanzania na kukuza uchumi wa ubunifu.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...