Na Pamela Mollel,Arusha.

CRDB Bank Plc imezindua rasmi Ripoti ya Mwaka 2025 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Arusha, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa wa benki hiyo unaotarajiwa kufanyika Mei 16, 2026 katika Ukumbi wa Simba ndani ya Arusha International Conference Centre (AICC)

Ripoti hiyo imeeleza kwa kina utendaji wa benki, mafanikio yaliyopatikana pamoja na hatua mbalimbali za ukuaji wa biashara na uendelevu zilizotekelezwa katika mwaka uliopita

Akizindua ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB Bank Plc, Profesa Neema Mori, amewataka wanahisa kuisoma kwa makini ili waweze kushiriki kikamilifu katika maamuzi yatakayofanyika kwenye mkutano mkuu ujao.

Prof. Mori amesema Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa utafanyika katika ukumbi wa Simba wa AICC pamoja na kupitia njia ya kidijitali, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa wanahisa wengi zaidi waliopo ndani na nje ya nchi

Aidha, amewakaribisha wanahisa wote kushiriki mkutano huo, akisema ni jukwaa muhimu la kujadili maendeleo ya benki pamoja na maamuzi yatakayosaidia kukuza taasisi hiyo kwa miaka ijayo

Akizungumzia Siku ya Uwekezaji kwa Wanahisa itakayofanyika Mei 15, 2026, Prof. Mori amesema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar

Amesema katika mkutano huo wanahisa watajadili na kuidhinisha agenda mbalimbali zikiwemo Ripoti ya Wakurugenzi, taarifa za hesabu zilizokaguliwa za mwaka 2025, pendekezo la gawio, uteuzi wa wakaguzi wa hesabu pamoja na uteuzi wa mjumbe mmoja huru wa bodi

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Plc, Abdulmajid Nsekela, amesema benki hiyo inaingia kwenye mkutano huo ikiwa na matokeo mazuri ya kifedha na kuendelea kuimarisha nafasi yake katika sekta ya fedha

Dkt. Nsekela amesema katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, benki hiyo imefanikiwa kurekodi faida baada ya kodi ya Shilingi bilioni 206, matokeo ambayo yametokana na maamuzi sahihi ya kimkakati, uongozi imara na kuendelea kuimarika kwa imani ya wanahisa na wawekezaji

Akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu ya “Vijana na Uwekezaji katika Hisa,” amesema CRDB Bank Plc inalenga kuhamasisha vijana kuona uwekezaji kama sehemu muhimu ya maisha yao ya baadaye

Amesema benki hiyo imeendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha vijana kujifunza kuhusu uwekezaji katika hisa na masoko ya mitaji ili wawe sehemu ya safari ya ukuaji wa benki hiyo na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...