Na Janeth Raphael MichuziTv Itigi - Singida

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameielekeza Sekta ya Ardhi kujitathmini kwa kina na kuchukua hatua za haraka kurekebisha changamoto zinazoikabili, akieleza kuwa imeendelea kuwa chanzo kikubwa cha migogoro katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza na wananchi wa Itigi mkoani Singida leo Dkt. Mwigulu amesema kumekuwa na ongezeko la migogoro ya ardhi inayotokana na wizi, udanganyifu na uzembe wa baadhi ya watendaji, hali ambayo imekuwa ikisababisha wananchi kugombana na hata kuvuruga mshikamano wa kijamii.

Amesema migogoro hiyo imekuwa ikiwakosesha wananchi haki zao za msingi na kuathiri maendeleo ya jamii, huku baadhi ya wananchi wakijikuta wakipoteza ardhi zao kutokana na mifumo isiyo na ufanisi pamoja na vitendo vya rushwa vinavyohusishwa na baadhi ya watumishi wasio waadilifu.

Waziri Mkuu amesisitiza kuwa sekta hiyo inapaswa kufanya maboresho makubwa yatakayorejesha imani ya wananchi kwa kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mwenye madai halali ya ardhi na kwamba serikali haitavumilia watendaji watakaobainika kushiriki vitendo vinavyozalisha migogoro hiyo.

Aidha, ameeleza kuwa ardhi ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla, hivyo ni lazima isimamiwe kwa uadilifu, uwazi na weledi ili kuondoa malalamiko yanayoendelea kujitokeza katika maeneo mbalimbali nchini.

Dkt. Mwigulu ameonya kuwa migogoro ya ardhi ikiendelea kuachwa bila kutatuliwa inaweza kuathiri umoja wa wananchi na kuleta uhasama usio wa lazima, akisisitiza kuwa kila taasisi inayohusika na usimamizi wa ardhi inapaswa kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria, kanuni na maslahi ya wananchi.

Aidha  amewataka viongozi na watendaji wa sekta hiyo kuhakikisha wanashughulikia kwa haraka kero za ardhi zinazowakabili wananchi ili kuimarisha amani, mshikamano na maendeleo ya taifa.



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...