WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuhakikisha Mradi wa Maji wa Miji 28 katika Mji wa Chemba unakamilika kwa wakati ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Wilaya ya Chemba.
“Wilaya ya Chemba ni moja ya wilaya zenye shida ya ukame na maji, lakini pia ni wilaya za uzalishaji, kwa hiyo tunahitaji sana mradi huu ukamilike haraka,” amesema.
Waziri Mkuu amesema hayo leo Jumapili, Mei 17, 2026 wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 katika Mji wa Chemba unaotekelezwa kupitia Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Chemba.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa Usambazaji Maji kutoka Wizara ya Maji, Eng. Charles Mafie amesema mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 11 unatarajiwa kuhudumia wananchi zaidi ya 18,141 wa Mji wa Chemba pamoja na vijiji vya Chemba, Chambalo, Kambi ya Nyasa, Gwandi, Paranga na Makamaka.
Amesema mradi huo umefikia asilimia 76 ya utekelezaji na unahusisha ujenzi wa visima vitatu vyenye uwezo wa kuzalisha maji lita 207,000 kwa saa, matenki ya kuhifadhi maji, kituo cha kusukuma maji pamoja na ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji yenye urefu wa kilomita 60.
Aidha, amesema mradi huo utaongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 37 ya sasa hadi asilimia 100 na kuongeza uzalishaji wa maji kutoka wastani wa lita laki moja na sabini kwa siku hadi kufikia zaidi ya lita milioni tatu kwa siku.
Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi M/s Megha Engineering and Infrastructure Limited (MEIL) chini ya usimamizi wa Mhandisi Mshauri WAPCOS Limited.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wakandarasi wanaotekeleza mradi huo kuhakikisha wanawalipa kwa wakati vijana, mafundi na vibarua wanaoshiriki katika utekelezaji wa kazi kupitia mikataba ya ushirikiano (subcontracting).
“Muendelee na kazi, lakini kila mnapopata fedha za mradi hakikisheni mnawalipa wanaofanya kazi pamoja nanyi. Vijana wetu waliopata subcontracting, mafundi na vibarua wote wapate malipo yao kwa wakati,” amesema.
Pia amesema Serikali imekuwa ikipokea malalamiko katika baadhi ya maeneo kuhusu miradi kukamilika huku baadhi ya watu waliohusika katika utekelezaji wake wakibaki wanadai malipo yao jambo ambalo halikubaliki.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema ana imani kubwa na usimamizi wa viongozi wa Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo akieleza kuwa usimamizi madhubuti una mchango mkubwa katika kuhakikisha miradi hiyo inaleta matokeo chanya kwa wananchi.




.jpeg)
.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...