-Dhamira ya Rais Samia kuboresha huduma bandari ya Dar sasa zinaonekana kwa vitendo

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

BAADA ya kuwa na kelele nyingi wakati Serikali ya Awamu ya Sita inatangaza kuingia mkataba na Kampuni ya kimataifa ya DP World hatimaye sasa kampuni hiyo imetimiza miaka miwili ikiendelea kutoa huuduma katika bandari ya Dar es Salaam kwa mafanikio makubwa.

Kwa kukumbusha tu DP World ilianza kutoa huduma katika Bandari ya Dar es Salaam Aprili 7,mwaka 2024 hivyo tayari imetimia miaka miwili na siku kadhaa.

Ni miaka miwili yenye mafanikio makubwa,miaka miwili yenye kuonesha dhamira njema ya Serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha huduma za bandari ya Dar es Salaam zinakuwa bora na kuendana na ushindani uliopo hasa za majirani zetu.

Bandari ya Dar es Salaam kwa muda mrefu huko nyuma  pamoja na sababu mbalimbali ukweli ilikuwa inalalamikiwa kutokuwa na ile kasi ya utoaji huduma hasa ya kushusha na kupakia makasha kwa maana ya makontena,lakini pia ucheleweshaji wa mizigo mchanganyiko.Sababu nyingine ni kuzubaa kwa huduma kwa ujumla.Zipo sababu nyingi hizo ni baadhi tu.Sijazungumzia ishu ya mapato.

Kutokana na sababu hizo na nyingine Serikali ya Awamu ya Sita iliona haja ya kuwa na Kampuni ya kimataifa ambayo inaweza kuondoa changamoto hizo ili sasa huduma ziwe bora na ndipo DP World alipopewa jukumu la kuendesha sehemu ya bandari hiyo.

Uamuzi ule wa Serikali ukaibua mambo mengi,uzushi nao ukapewa nafasi kubwa .Si unajua tena katika nchi hii kuna watu wanaamini uzushi kuliko ukweli.Ndio wakati tuliosikia eti bandari ya Dar es Salaam imeuzwa .Kha ! Ila ndio Tanzania yenye watu na viatu.

Leo hii miaka miwili ya uwepo wa DP World huduma zimekuwa bora sana ,msongamano wa meli katika eneo la bandari ya Dar es Salaam halipo tena,muda wa kushusha na kupakia mzigo umepungua, maboresho ya gati na maeneo mengine yanaendelea, mapato yameongezeka.

Siku za karibuni Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF) lilifanya ziara katika bandari ya Dar es Salaam lengo kuona shughuli zinazofanywa na DP World baada ya kuwa imetimiza miaka miwili.

Hakika kuna maboresho makubwa sana,kazi inaendelea na ile Kazi na Utu imepewa nafasi kubwa. Kwa huduma za DP World wale waliokuwa wanazusha wakati ule leo wanaona aibu .Ndio.

Katika ziara ya Jukwaa la Wahariri Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha DP World Elitunu Malamia ametumia nafasi hiyo kuelezea safari ya miaka miwili ya uwepo wao katika utoaji huduma hasa katika gati namba 0 hadi gati namba 7.

“Tumetimiza miaka miwili na siku kadhaa na katika makubaliano yetu ya kuweka dola bilioni 250 tayari tumeshawekeza dola bilioni 125 ambapo tumevuka katikati ya lengo.

“Tunashukuru soko linakwenda vizuri na linaonesha uhakika katika huu uwekezaji kwa meli kubwa zaidi,mpya zaidi na mzigo mwingi zaidi kuja katika bandari yetu ya Dar es Salaam.

“Kwenye yard uwekezaji ambao tumeufanya na tunaendelea mpaka sasa ni maboresho yakiwemo uwekaji wa zege mpya ,na maeneo mengine yanajengwa kabisa hasa katika eneo la kuweka mzigo mchanganyiko.”

Pia anaeleza kuwa DP World imeweka zege mpya kabisa kwa ajili ya kuweka mizigo kama machuma ,nondo pamoja na coil.“Maboresho yanaendelea katika maeneo mbalimbali na tunaendelea na ujenzi wakati huduma zikiendelea.”

Mbali ya kuboresha miundombinu DP World imeendelea kuongeza vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuboresha utoaji huduma katika bandari hiyo.Ununuzi wa vifaa kama RTG umeendelea.Wameongeza TT bandarini hapo.

Akifafanua zaidi anaeleza kwenye uwezo  wa kibandari gati namba moja mpaka namba nne wanauwezo wa kuweka meli kubwa tatu na ndogo moja wakati gati namba tano mpaka saba kutokana na ukubwa wa meli zinahudumiwa mbili.

“Eneo lingine ambalo tumeliboresha sana katika miaka miwili ambayo tumekuwepo ni matumizi ya TEHAMA.Tumetambulisha mfumo wa kısasa wa uendeshaji wa bandari.

“Tunaweza kupata taarifa za makasha ya shehena kwa wakati yaani mubashara,pale mzigo unapashuka kuna taarifa zinatumwa kwenda katika vyombo husika vinavyohitaji taarifa hizo kama TRA na wengineo 

“Pia muingiliano katı ya mifumo yetu na mifumo ya TRA tumeboresha kwa maana kwamba inasoma vizuri zaidi kuliko awali.Maboresho ya TEHAMA vinapunguza muda unaotumika katika ukomboaji wa shehena.Hakuna mambo ya kukimbizana na karatasi.”

Kwenye utendaji amesema ukilinganisha mwaka 2024 na zilizofanyika mwaka 2025 taarifa za robo ya kwanza ya mwaka huu wamevuka lengo kwa ongezeko la asilimia 99.”Ongezeko hilo ni kwa bandari ile ile kwa nafasi ile ile kwa mageti yaleyale.”

Aidha amesema wamejenga geti jipya mwaka huu na matokeo yake yameanza kuonekana.

Pamoja na hayo ameeleza bandari ya Dar es Salaam kama bandari ukiacha eneo linaloendeshwa na DP World kuna eneo linaloendeshwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA) halafu kuna gati namba nane ,tisa 10,11 ni magati yanayohudumia mzigo wa kontena yenyewe yanaendeshwa na muwekezaji mwingine.

“Mafanikio haya ninayoeleza zinahusu DP World ,hivyo tunapozungumzia kuongezeka kwa kupakia na kushusha makontena,mizigo mchanganyiko na magari tunazungumzia upande wetu.”amesema na kusisitiza wamekuwa na mafanikio makubwa.

Pamoja na hayo amesema kuimarika kwa Bandari ya Dar es Salaam imesaidia kuongeza mapato yanayotokana na ushuru wa forodha na ndio maana hata Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) imekuwa ikivunja rekodi ya ukusanyaji mapato kwani mchango wa bandari katika mapato ni mkubwa.

“Kikubwa sana ambacho ni muhimu kufahamu pia kuanzia mwaka 2025 TRA wamekuwa hawana shida kuvunja rekodi zao za makusanyo.Mnajua kwanini? Ni bandari ya Dar es Salaam .

“Makusanyo yote anayokusanya TRA nchi nzima asilimia 40 yanatokana na forodha.Forodha ni ushauri unaokusanywa katika mipaka au bandari na bandari ya Dar es Salaam inachangia takribani  asilimia 30, hivyo kadri tunavyofanya kazi zaidi ya kuhudumia mizigo ndivyo tunavyofanya kipatikane cha kukusanya hayo mapato.

Tuwasiliane mtu wangu 

0713833822






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...