-Kozi mpya kwa wakufunzi zaanza kutolewa rasmi,Mkurugenzi wa Chuo atoa neno 

Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV

CHUO Cha  udereva Cha Future World kilichopo eneo la Chanika wilayani Ilala jijini Dar es Salaam kimeendelea kuwanoa madereva wa magari ya abiria na mizigo lengo likiwa kuwajengea uelewa wa elimu ya usalama barabarani ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kutokomeza ajali za barabarani nchini.

Madereva wanaofika katika chuo hicho ni kwa ajili ya  kupata mafunzo zaidi ya udereva sambamba na kupatiwa elimu ya usalama barabarani ambapo wamekuwa wakitoka katika mikoa mbalimbali nchini.

Akizungumza  Mei 26,2026 wakati wa kupokea madereva waliojiunga na chuo hicho,madereva waliomaliza masomo yao kwa kufanya mihatihani pamoja na kutambulisha kozi mpya ya  mafunzo maalum kwa wakufunzi wa udereva ,Mkurugenzi Mtendaji na Mmiliki wa chuo hicho Robert Mkolla ametumia nafasi kueleza kwa kina sababu za ajali za barabarani hatua ambazo chuo kinazichukua kukomesha ajali hizo.

Amefafanua kuna sababu tatu ambazo ndizo zimekuwa chanzo cha ajali  za barabarani na ili kuondoa sababu hizo  ni lazima  dereva kupatiwa elimu na ndio maana chuo hicho kimekuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa madereva nchini.

“Tafiti zinaonesha ajali nyingi za barabarani zinatokana na makosa ya kibinadamu na hasa makosa ya dereva na sababu zinazosababisha ajali hizo ni uzembe, upuuzaji na kutokujua.

“Hakuna binadamu mwenye akili timamu asiyejua madhara ya ajali ,kinachosababisha ajali  ni kutojua ,kupuuza au kuzembea,”amesema na kufafanua sababu hizo zote zinaondolewa kwa dereva kupatiwa mafunzo na elimu ya usalama barabarani.

Kuhusu chuo hicho amesema kimeendelea kuwa Chuo kinachopika madereva ambao wanaweza kuendesha magari ndani na nje ya Tanzania kwani mbali ya kupata mafunzo ya udereva na elimu ya usalama barabarani chuo kina moundombinu yote muhimu sambamba na uwepo wa magari ya kutosha kufundishia huku pia teknolojia katika ufundishaji ikipewa kipaumbele.

Kwa upande wa madereva ambao wanapatiwa mafunzo katika chuo hicho akiwemo Erasto John na George Steven wamesema wamefika kupata mafunzo hayo kwa sababu katika zama hizi hakuna tena ujanja ujanja na Serikali imesimama imara katika kusimamia sheria za usalama barabarani sambamba na kuwa na madereva waliopata mafunzo ya udereva katika vyuo vinavyotambulika.

Wamesema kutokana  na hali hiyo ndio wamelazimika kufika katika chuo hicho ili kupata elimu ya usalama ya barabarani na hasa katika udereva wa kujihami ambapo udereva huo ndio unaepusha ajali za barabarani.

Wameeleza kabla ya kwenda kusoma walikuwa wanaendesha gari bila kuwa na uelewa wa kutosha hasa kutafsiri alama za barabarani lakini kwa sasa wamefahamu na wanauelewa mkubwa kuhusu udereva na sheria zake.

Wakati huo huo wakufunzi Egnas Bethod na Elbariki Juma ambao wametoka vyuo tofauti vya dereva na wapo katika Chuo cha Future World kwa ajili ya kuongezewa ujuzi kupitia kozi ya ukufunzi  wamesema kuna mabadiliko mengi yamekuwa yakitokea katika taaluma ya udereva .

Wamefafanua kutoka mwaka jana hadi sasa mfumo umekuwa wa utoaji leseni umekuwa ukibadilika hasa kwa mamlaka kuweka vigezo vya utoaji leseni.

“Zamani mtu alikuwa anaenda chuo hata kwa siku moja au mbili na anapewa leseni ya udereva.Wapo pia waliokuwa wanapata leseni kwa kuletewa na ndugu zao lakini kwa sasa hakuna njia za mkato,kwa siku hizi lazima ufuate utaratibu uliowekwa na Serikali, hivyo lazima sisi tunaofundisha madereva tuendelee kupata maarifa mapya kwa ajili ya kutuwezesha kuwafundisha madereva.”

Wameongeza kwa siku hizi ili chuo cha udereva kiwe na hadhi ya kutoa cheti kwa wanafunzi lazima wakufunzi na wenyewe wawe na vigenzo ambavyo usajili wake umetoka Jeshi la Polisi , hivyo imewalazimu nao kurudi darasani ili vyuo vyao viwe na sifa ya kutoa vyeti na wanafunzi ambao ni madereva kupata leseni.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...