Na Janeth Raphael MichuziTv Bungeni - Dodoma

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Paschal Katambi Patrobass amesema Serikali imeendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa raia pamoja na mali zao kupitia operesheni mbalimbali zinazofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama nchini.

Katambi ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, Wizara kupitia Jeshi la Polisi imeendelea kufanya doria, misako na operesheni maalum zenye lengo la kubaini, kuzuia na kutanzua vitendo vya uhalifu katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi umechangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kuwepo kwa hali ya amani na utulivu nchini, jambo ambalo limewawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii kwa utulivu.

Aidha, Katambi amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu utekelezaji wa falsafa ya Polisi Jamii ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika mapambano dhidi ya uhalifu.

Katika takwimu alizowasilisha bungeni, Katambi amesema makosa makubwa ya jinai yaliyotolewa taarifa katika vituo vya Polisi nchini yamepungua katika kipindi hicho.

Amesema kuanzia Julai 2025 hadi Aprili 2026 jumla ya makosa makubwa ya jinai 39,027 yaliripotiwa katika vituo vya Polisi, ikilinganishwa na makosa 40,022 yaliyorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2024/2025.

Katambi alieleza kuwa kupungua kwa makosa hayo kunatokana na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi pamoja na ushirikiano wa jamii katika kubaini na kuzuia vitendo vya uhalifu kabla havijatokea au kusababisha madhara makubwa.

Akifafanua zaidi kuhusu aina za makosa yaliyorekodiwa, Waziri huyo alisema makosa 9,603 yalikuwa dhidi ya binadamu, makosa 13,986 yalihusiana na maadili ya jamii, makosa 14,794 yalikuwa ya kuwania mali huku makosa 644 yakihusiana na uhalifu wa kifedha.

Waziri Katambi alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya usalama, kuongeza uwezo wa vyombo vya dola pamoja na kuendeleza ushirikiano na wananchi ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa salama na yenye utulivu wakati wote.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...