Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma 

Serikali imetangaza kuwa ipo katika hatua za mwisho za kuandaa mfumo wa kisheria pamoja na sera maalum zitakazosimamia huduma za upandikizaji wa viungo, ikiwa ni jitihada za kurasimisha na kuimarisha sekta hiyo muhimu ya afya nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la kimataifa la kisayansi lililoandaliwa na Hospitali ya Benjamin Mkapa lililolenga kujadili sera, mwelekeo na mikakati ya kuendeleza huduma za upandikizaji viungo, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, alisema maandalizi hayo yanatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba mwaka huu.

Amesema  kuwa uwepo wa sera na sheria hizo utaweka misingi imara ya utoaji huduma hizo kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa, hali itakayosaidia kuongeza ufanisi na usalama kwa wagonjwa.

Dkt. Magembe alibainisha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, jambo linalowezesha wagonjwa wengi kupata matibabu ya hali ya juu ndani ya nchi badala ya kusafiri nje ya mipaka.

Alitaja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na huduma za upandikizaji wa uloto kwa wagonjwa wa saratani ya damu pamoja na upandikizaji wa figo, huku akieleza kuwa mipango inaendelea ya kuanzisha huduma za upandikizaji wa ini na moyo katika siku za usoni.

Pamoja na mafanikio hayo, Dkt. Magembe alisisitiza umuhimu wa wananchi kujiunga na mifumo ya bima ya afya, akieleza kuwa huduma za upandikizaji viungo zina gharama kubwa ambazo si rahisi kumudu bila bima.

Alifafanua kuwa gharama za upandikizaji wa uloto zinaweza kufikia shilingi milioni 75, huku upandikizaji wa figo ukigharimu takribani shilingi milioni 40, hali inayofanya uwepo wa bima kuwa nguzo muhimu kwa wananchi wengi.

Kwa mujibu wake, hadi sasa zaidi ya wagonjwa 147 wamefanikiwa kufanyiwa upandikizaji wa uloto na figo hapa nchini, hatua inayopunguza utegemezi wa matibabu nje ya nchi na kuokoa gharama kubwa za usafiri na matibabu.

Aidha, alibainisha kuwa wagonjwa wa figo wanaohitaji huduma ya kuchuja damu hulazimika kufanya hivyo mara kadhaa kwa wiki, jambo linaloambatana na gharama na changamoto kubwa za maisha, hivyo bima ya afya inaweza kuwa suluhisho muhimu kwao.

“Ni muhimu wananchi wakaona umuhimu wa bima ya afya kama wanavyochukulia bima ya magari, kwa sababu inasaidia kukabiliana na gharama kubwa za matibabu,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamini Mkapa, Profesa Abel Makubi, aliipongeza serikali kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya, akisema hatua hiyo imewezesha kuboreshwa kwa huduma za kibingwa nchini.

Ameeleza kuwa kongamano hilo limewakutanisha zaidi ya wataalamu 150 wa afya kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha ujuzi katika huduma za kisasa za matibabu.

Profesa Makubi aliongeza kuwa hospitali hiyo imejikita katika kuendeleza huduma za upandikizaji viungo na itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha huduma hizo zinapanuka zaidi.

Kwa upande wa wanufaika, baadhi ya wagonjwa waliopatiwa huduma hizo walieleza mafanikio yao, wakisema matibabu hayo yamebadilisha maisha yao kwa kiwango kikubwa.

Miongoni mwao ni Richard Masimba, aliyefanyiwa upandikizaji wa figo miezi sita iliyopita, ambaye alieleza shukrani zake kwa madaktari na serikali kwa kumpa nafasi ya kuendelea kuishi maisha ya kawaida.

Naye Nasra Gwota alisema kabla ya kupandikizwa uloto alikuwa akisumbuliwa mara kwa mara na kulazimika kukosa masomo, lakini kwa sasa anaendelea vizuri na kurejea katika shughuli zake za kila siku.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...