Na Janeth Raphael- MichuziTv
Serikali imesema sekta ya ufugaji nyuki nchini imepiga hatua kubwa kimataifa baada ya mauzo ya asali kuongezeka kwa kiwango kikubwa na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika masoko ya dunia pamoja na taasisi za kimataifa za uhifadhi.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akiwasilisha Bungeni jijini Dodoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2026/27 ambapo amesema kiwango cha asali kinachouzwa nje ya nchi kimeongezeka kutoka tani 951.6 mwaka 2024 hadi tani 1,596.8 mwaka 2025 sawa na ongezeko la asilimia 67.85 huku thamani ya mauzo hayo ikipanda kutoka Shilingi bilioni 11.4 hadi Shilingi bilioni 19.2 sawa na ongezeko la asilimia 68.4, hatua inayotokana na juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya ufugaji nyuki katika kuboresha uzalishaji, kuongeza ubora na kuhakikisha asali ya Tanzania inakidhi viwango vya kimataifa.
Dkt. Kijaji amesema mafanikio hayo yamechangiwa pia na utekelezaji wa mpango madhubuti wa kudhibiti mabaki ya kemikali katika asali ambao umeiwezesha bidhaa hiyo kuendelea kufikia wastani wa asilimia 97 wa kufuata viwango vya Umoja wa Ulaya kwa miaka mitatu mfululizo, jambo lililoongeza uaminifu wa asali ya Tanzania katika soko la dunia na kufungua fursa mpya katika nchi mbalimbali zikiwemo Marekani, nchi za Umoja wa Ulaya, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na China, huku kwa mara ya kwanza asali ya Tanzania ikiingia rasmi katika soko la Uingereza baada ya kukidhi vigezo vya soko hilo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kijaji amesema Tanzania imeendelea kuimarisha hadhi yake kimataifa katika uhifadhi na usimamizi wa maeneo ya Urithi wa Dunia baada ya kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2025 hadi 2029 ambapo kupitia nafasi hiyo Tanzania sasa ni miongoni mwa nchi 21 kati ya 195 duniani zinazounda chombo hicho cha juu cha UNESCO kinachohusika na maamuzi ya uhifadhi wa maeneo ya Urithi wa Dunia na hivyo kuipa nchi nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika maamuzi ya kuongeza au kuondoa maeneo katika orodha hiyo pamoja na kuimarisha sera za kimataifa za uhifadhi.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...