Na Janeth Raphael, Michuzi TV Bungeni – Dodoma
Mbunge wa Jimbo la Makete mkoani Njombe, Festo Sanga, amesema Tanzania imeendelea kuwa kivutio na kutazamwa kwa jicho la husuda na baadhi ya mataifa kutokana na hali ya amani, utulivu na mshikamano uliopo nchini, hali ambayo imekuwa ikichochea baadhi ya watu kufanya vitendo vinavyoweza kuleta mtafaruku na kuhatarisha usalama wa taifa.
Mbunge huyo ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akichangia hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa mifumo ya ulinzi na usalama kuanzia ngazi za chini kabisa za jamii.
Katika mchango wake, Sanga alitaka kurejeshwa kwa mfumo wa nyumba kumi, akieleza kuwa mfumo huo utasaidia kutambua watu wanaoingia na kutoka katika maeneo mbalimbali nchini na hivyo kurahisisha udhibiti wa uhalifu pamoja na matukio yanayoweza kuhatarisha usalama wa wananchi.
Amesema kuwa katika kipindi hiki ambacho teknolojia na mwingiliano wa watu umeongezeka kwa kasi, ipo haja ya kuwa na utaratibu madhubuti wa kufahamu taarifa za wakazi katika maeneo mbalimbali ili kuimarisha ulinzi shirikishi.
“Ni lazima kama nchi turejeshe mfumo wa nyumba kumi ili tuweze kufahamu nani anaingia na nani anatoka katika maeneo yetu. Tanzania ina amani kubwa, lakini kuna watu wanaotamani kuona nchi yetu ikiingia kwenye migogoro na machafuko, hivyo hatupaswi kubeza masuala ya usalama,” alisema Sanga.
Aidha, mbunge huyo aliibua hoja kuhusu usajili holela wa laini za simu, akisema tatizo hilo limekuwa chanzo kikubwa cha utapeli na wizi unaowaumiza wananchi wengi nchini.
Alisema bado kuna watu wanafanikiwa kusajili laini za simu katika mazingira yasiyo rasmi na bila kufuata taratibu stahiki, jambo ambalo limekuwa likitumiwa na wahalifu kufanya utapeli wa fedha pamoja na uhalifu mwingine wa kimtandao.
“Suala la usajili holela wa laini za simu limekuwa kubwa sana. Watu wanaibiwa fedha kila siku kupitia simu na matapeli wanatumia laini zilizosajiliwa kiholela. Hili suala lichukuliwe kwa uzito mkubwa,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, aliitaka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kushirikiana kwa karibu na vyombo vya usalama ili kudhibiti vitendo hivyo na kuhakikisha hakuna laini inayosajiliwa bila utambulisho sahihi wa mhusika.
Mbunge huyo pia alipongeza juhudi za serikali katika kuendelea kuboresha mifumo ya utambuzi wa vyombo vya moto na taarifa za wamiliki wa magari, akisema hatua hiyo imesaidia kwa kiwango kikubwa katika kusaidia ufuatiliaji wa wahalifu.
Hata hivyo, alisema bado kuna mapungufu katika maeneo ya nyumba za kulala wageni na mahotelini ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakitumia majina yasiyo yao wanapofikia huduma hizo, hali inayoweza kuhatarisha usalama wa taifa.
Amesema ipo haja ya serikali kuweka mfumo wa kisasa wa uhakiki wa taarifa za wageni katika mahotel, nyumba za wageni na nyumba za kupanga, ambapo kila anayefikia huduma hizo atalazimika kutumia kitambulisho rasmi kama NIDA, pasipoti au kitambulisho cha mpiga kura ili taarifa zake ziweze kuhakikiwa moja kwa moja kwenye mfumo.
“Leo kuna watu wanaenda kwenye nyumba za wageni, wanaandika majina ambayo si yao, wanalala na kuondoka bila kufahamika. Ni lazima tuwe na mifumo ya verification kwenye mahotel na nyumba za kulala wageni ili jina la mtu lionekane sahihi kwenye mfumo,” amesema.
Sanga ameongeza kuwa hata kwa nyumba zinazopangishwa, ni muhimu kuwepo kwa mfumo wa uhakiki wa wapangaji ili kila anayepanga nyumba awe ametambulika rasmi, jambo litakalosaidia kupunguza vitendo vya kihalifu vinavyofanywa kwa kujificha katika makazi ya watu.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, kuimarishwa kwa mifumo ya utambuzi na uhakiki wa taarifa za wananchi kutasaidia kuongeza usalama wa taifa, kupunguza uhalifu wa mtandao pamoja na kulinda amani na utulivu ambao Tanzania imeendelea kujivunia kwa miaka mingi.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...