Na Janeth Raphael MichuziTv
Serikali imeelezwa kuwa migongano kati ya binadamu na wanyamapori imeendelea kuwa moja ya changamoto kubwa katika Sekta ya Maliasili na Utalii, huku karibu nusu ya halmashauri zote nchini zikikumbwa na tatizo hilo linalosababisha vifo, majeraha na uharibifu mkubwa wa mali za wananchi.
Hayo yameelezwa bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mzava, wakati akiwasilisha taarifa ya Kamati kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na maoni ya Kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Mzava amesema licha ya mafanikio yanayoendelea kupatikana katika sekta ya maliasili na utalii, migongano kati ya wananchi na wanyamapori bado inaathiri maeneo mengi nchini, hasa yale yanayopakana na hifadhi za taifa na mapori ya akiba.
Amesema kati ya halmashauri 184 zilizopo nchini, halmashauri 91 sawa na asilimia 49.5 zinakabiliwa na changamoto hiyo, huku tembo wakitajwa kuwa chanzo kikubwa cha migogoro hiyo kwa kiwango cha asilimia 80.
Kwa mujibu wa Kamati hiyo, wanyamapori wengine wanaosababisha migongano hiyo ni pamoja na mamba, viboko, nyumbu, ngedere na nyani, ambao wamekuwa wakivamia maeneo ya wananchi na kusababisha madhara mbalimbali.
“Madhara yanayotokana na migongano hii ni pamoja na vifo vya wananchi, ulemavu wa muda au wa kudumu kutokana na mashambulizi ya wanyama, pamoja na uharibifu wa mali ikiwemo mazao, nyumba, miundombinu ya maji na barabara,” amesema Mzava.
Aidha, Kamati imebainisha kuwa baadhi ya sababu zinazochochea kuongezeka kwa migongano hiyo ni kutokuwepo au kutotekelezwa ipasavyo kwa mipango bora ya matumizi ya ardhi, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na ongezeko la mimea vamizi ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa.
Kutokana na hali hiyo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto hiyo ikiwemo kuongeza doria za kudhibiti wanyamapori, kununua pikipiki za doria, kujenga vizimba vya kudhibiti wanyama wakali na waharibifu pamoja na kujenga vituo vya askari wa wanyamapori.
Hatua nyingine zilizotajwa ni uchimbaji wa visima na mabwawa ndani ya maeneo ya hifadhi ili kupunguza wanyama kutoka nje kutafuta maji, pamoja na uwekaji wa visukuma mawimbi kwa baadhi ya wanyama viongozi wa makundi ili kurahisisha ufuatiliaji wao.
Kamati hiyo pia imeeleza kuwa Serikali imeendelea na zoezi la uvunaji wa baadhi ya wanyamapori wanaoleta madhara makubwa kwa wananchi ambapo katika mwaka wa fedha 2025/2026 jumla ya tembo 100, viboko 197, fisi 171 pamoja na mamba 153 walivunwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kupunguza athari za migongano hiyo.
Mzava amesema Kamati itaendelea kuisimamia Serikali kuhakikisha mikakati ya kudhibiti migongano hiyo inaongezwa nguvu ili kulinda maisha ya wananchi sambamba na kuhifadhi rasilimali za wanyamapori ambazo ni muhimu kwa uchumi wa taifa kupitia sekta ya utalii.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...