Na Janeth Raphael MichuziTv- Bungeni Dodoma
Mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Paul Mnzava, ameitaka Serikali kuongeza kasi ya maboresho na upanuzi wa miundombinu ya barabara zinazounganisha Bandari ya Tanga na maeneo mbalimbali ya nchi, akisisitiza kuwa ufanisi wa bandari hiyo hautakuwa na maana kamili bila barabara imara za usafirishaji wa mizigo.
Akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma, Mnzava amesema maboresho yanayoendelea katika Bandari ya Tanga yameongeza kiasi kikubwa cha shehena ya mizigo, hatua ambayo ni mafanikio makubwa kwa uchumi wa taifa.
Hata hivyo, amesema mafanikio hayo yanapaswa kuendana sambamba na uboreshaji wa barabara kuu zinazopeleka mizigo kutoka bandari hiyo kwenda maeneo mbalimbali ya nchi, ili kuhakikisha ufanisi wa huduma na kupunguza gharama za usafirishaji.
“Uwekezaji mkubwa uliofanyika kwenye Bandari ya Tanga unapaswa kuendana na uboreshaji wa barabara. Bila hivyo, tunapoteza maana ya maendeleo haya,” amesema Mnzava.
Ameeleza kuwa baadhi ya barabara muhimu katika mtandao huo zimechoka na zimepitwa na muda wa matumizi yake, huku Serikali ikiwa imekuwa ikitoa ahadi za kuzifanyia matengenezo kwa muda mrefu bila utekelezaji wa haraka unaotarajiwa.
Aidha, amemtaka Waziri wa Ujenzi kufafanua kwa kina mikakati ya Serikali kuhusu upanuzi na ukarabati wa barabara ya Tanga–Segera pamoja na Segera–Chalinze, ambazo ni njia muhimu zinazounganisha mikoa ya Kaskazini na maeneo mengine ya nchi.
Mnzava amesema barabara hizo si tu za kiuchumi kwa mikoa ya Kaskazini, bali zinahudumia Watanzania wengi kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo Tanga, Morogoro, Singida na Dodoma, ambao wanategemea miundombinu hiyo kwa shughuli za usafirishaji wa mizigo na biashara.
Ameongeza kuwa ili barabara hizo ziweze kutimiza lengo la kuongeza ufanisi wa Bandari ya Tanga, ni lazima Serikali iweke wazi hatua zilizochukuliwa na muda wa utekelezaji wa miradi hiyo muhimu ya kimkakati.
“Ni muhimu Serikali kueleza wazi hatua zilizofikiwa na mipango ya muda mfupi na mrefu kuhusu ujenzi na upanuzi wa barabara hizi,” amesisitiza.
Katika hitimisho lake, Mnzava ametoa wito kwa wananchi wa maeneo yanayonufaika na barabara hizo kushirikiana pamoja katika kuunga mkono maendeleo ya miundombinu hiyo, akisema ni chachu ya ukuaji wa uchumi na ustawi wa taifa kwa ujumla.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...