Na Karama Kenyunko, Michuzi TV

SHIRIKA lisilo la Kiserikali la masuala ya Afya ya Uzazi, MSI Tanzania, limeingiza rasmi Tuzo ya Uandishi wa Habari za Afya ya Uzazi katika Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2025, hatua inayolenga kuhamasisha uandishi wa habari za afya wenye manufaa kwa jamii.

Tuzo hiyo ni miongoni mwa makundi mapya yaliyoanzishwa mwaka huu na Baraza la Habari Tanzania (MCT), ikiwa ni sehemu ya maboresho yanayolenga kuendana na mabadiliko ya mazingira ya habari na kuhimiza uandishi wenye utaalamu maalumu.

Hatua hiyo imetangazwa leo Mei 28, 2026 wakati MCT ikiongeza wateule 12 wa EJAT 2025, hatua iliyopanua orodha ya waandishi wa habari na taasisi zinazotambuliwa kwa umahiri wa kitaaluma, maadili ya uandishi na mchango kwa jamii.

Miongoni mwa wateule hao ni Julius Maricha wa The Citizen, Halima Mlacha wa Habari Leo, Hamadi Rashid wa The Loyal Media na UN Radio, Leonard Mubale wa TriGen Media, Philip Mwihava wa Clouds FM na Manyerere Jackton wa Jamhuri Media.

Kwa upande wa taasisi za habari, Azam Media, Nukta Africa, Mwananchi Newspaper, The Guardian Newspaper, Tanzania Standard Newspapers (TSN) na Jamhuri Newspaper zimetajwa kuingia hatua ya mwisho ya tuzo hizo.

Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest Sungura, amesema mfumo ulioboreshwa wa tuzo hizo unalenga kuongeza uwakilishi mpana zaidi, hususan katika uandishi wa habari za kidijitali, taarifa za mikoani na miradi ya uchunguzi wa habari.

Mbali na Tuzo ya Afya ya Uzazi, makundi mengine mapya ni Tuzo ya Uandishi wa Habari za Elimu ya Uwezo Tanzania, Tuzo ya Mahojiano Bora ya Mwaka, Tuzo ya Taasisi ya Habari Inayozingatia Sheria kwa Ubora wa Mwaka, Tuzo ya Taasisi ya Habari Yenye Utaalamu Maalumu wa Mwaka, Tuzo ya Uhifadhi ya Mwalimu Julius Nyerere pamoja na Tuzo ya Kijana Chipukizi.

Mkurugenzi Mkazi wa MSI Tanzania, Patrick Kinemo, amesema taasisi hiyo imekuwa ikisaidia programu za afya ya uzazi tangu mwaka 1989 kwa kushirikiana na Wizara ya Afya katika kuboresha huduma za uzazi wa mpango, hasa maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma.

Amesema MSI inaamini mchango wa vyombo vya habari ni muhimu katika kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi kuhusu afya ya uzazi.

Kwa mujibu wa Kinemo, katika kipindi cha miaka minne iliyopita ushirikiano kati ya MSI na MCT umewezesha mafunzo kwa wanahabari 30 na kuchangia kuandaliwa kwa zaidi ya habari 100 kuhusu afya ya uzazi zilizofikia wananchi na watunga sera.
Alisema ushirikiano huo umeongeza uelewa wa jamii kuhusu huduma za afya ya uzazi na kusaidia wananchi wengi, hususan wa maeneo ya mbali, kupata huduma muhimu.

Washindi wa EJAT 2025 wanatarajiwa kutangazwa kesho Mei 29 katika hafla itakayofanyika Hoteli ya Four Points by Sheraton jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkazi wa MSI Tanzania, Patrick Kinemo akizungumza wakati wa kutangaza kuingizwa kwa Tuzo ya afya ya Uzazi katika tuzo za EJAT 2025 Zimazotarajiwa kutolewa kesho Mei 29, 2026 jijini Dar es Salaam.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...