Na Seif Mangwangi, Michuzi TV, Karatu

SERIKALI imesema itaendelea kuwalinda wawekezaji wa ndani pamoja na kuunga mkono uwekezaji wowote unaofanywa na wawekezaji hao kwa lengo la kutoa huduma za kijamii.

Hayo yameelezwa leo 29 Mei 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Karatu Lameck Karanga katika hafla ya uzinduzi wa kituo kipya ya mafuta cha Orxy kitakachokuwa kikiendeshwa chini ya kampuni ya halyaz.

DC Karanga amesema ujenzi wa kituo hicho cha mafuta ni muendelezo wa maono ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wawekezaji wa ndani wanajengewa mazingira mazuri Ili waweze kufanya biashara.

Amesema Karatu ndio lango kuu la utalii hivyo ujio wa kituo hicho kutasaidia wasafirishaji kupata nishati ya mafuta kwa urahisi na uhakika kwa kuwa bidhaa za kampuni hiyo zinaaminika katika ukanda wa Afrika na duniani kote.

"Kwa niaba ya Wilaya niwapongeze sana kwa uwekezaji huu, mbali ya kutuletea kituo bora lakini mmeanza na kutengeneza mazingira hasa ya bustani nzuri hapo mbele ya kituo chenu, hii inaonyesha ni namna gani mmekuja Karatu Kwa faida," amesema na kuongeza:

"Orxy wameonyesha usafi wa mazingira nje ya kituo cha mafuta na niwaombe watu wa Benki na wenyewe waige mfano huu ni utalii mzuri na kuonyesha wilaya ya karatu ni safi na kuwa na mazingira mazuri," amesema.

Aidha DC Karanga amewataka wananchi wa mji wa Karatu kuiga mfano wa kampuni ya Halyaz kufungua taasisi kama hizo Ili kusaidia jamii kupata ajira lakini pia Serikali kupata kodi. 

Mkurugenzi wa kampuni ya Halyaz inayoendesha kituo hicho cha mafuta cha Orxy Karatu, Ally Abdulrazak amesema ujenzi wa kituo hicho ni matokeo ya maono kwamba karatu inastahili huduma bora za nishati.

Amesema aliamua kuingia ubia na kampuni ya Orxy kufungua kituo hicho cha mafuta kwa kuwa ndio kampuni ambayo imekuwa ikitoa  mafuta safi na salama kwa magari aina tofauti tofauti.

Abdulrazak amesema wateja watakaofika kupata huduma katika kituo hicho watapata huduma zenye ubora wa kimataifa kwa kuwa Wafanyakazi wake wanaujuzi wa hali ya juu lakini pia huduma zote zinaendeshwa kwa kuzingatia ubora.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Orxy Tanzania, Meneja wa fedha wa kampuni hiyo, Greyson Francis amesema uzinduzi wa kituo hicho cha mafuta cha Orxy Karatu ni sehemu ya ndoto za kampuni hiyo kuendelea kupanua huduma zake Kwa jamii.

Amesema kampuni ya Orxy imesambaa katika nchi 19 barani Afrika na hapa nchini imeshasambaa mikoa yote na hivi karibu itazindua vituo viwili vya mafuta Jijini Dar es Salaam.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...