Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, amesisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya nishati kwa wananchi ili kupunguza hatari ya majanga ya moto wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wazima Moto Duniani, yaliyofanyika Mei 4, katika viwanja vya soko kuu Manispaa ya Songea.
Ameeleza kuwa ni muhimu kwa wananchi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa mifumo ya umeme katika makazi yao ili kuhakikisha usalama wa familia na mali zao, aidha amewahimiza kutumia vifaa vya umeme vilivyokaguliwa na kuepuka matumizi holela ya nishati ambayo yanaweza kusababisha majanga.
Ameongeza kuwa suala la usalama si jukumu la Jeshi la Zimamoto pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi, ameeleza kuwa ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ni muhimu katika kuzuia na kudhibiti matukio ya moto kabla hayajaleta madhara makubwa.
Amelihimiza Jeshi la Zimamoto na uokoaji, kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa bidii, weledi na uaminifu, amesema serikali ya Mkoa wa Ruvuma itaendelea kushirikiana nao kwa karibu, ikiwemo kuboresha mazingira ya kazi na kutoa mafunzo zaidi ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ruvuma Melania Nyabwinyo, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuliwezesha jeshi hilo kutekeleza majukumu yake bila vikwazo.
Amebainisha kuwa serikali imefanikiwa kutoa mitambo ya kisasa, kuongeza idadi ya watumishi pamoja na kuboresha miundombinu kupitia ujenzi na ukarabati wa vituo vya zimamoto.



.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...