-Naibu Waziri Kwagilwa aahidi kufanya ziara katika halmashauri 184 kukagua zoezi hilo


Na Ashura Mohamed - ARUSHA

Serikali imesema haitamuonea haya mtu yeyote atakayefanya maigizo katika zoezi la upandaji miti nchini, ikieleza kuwa zoezi hilo ni muhimu kwa mustakabali wa mazingira.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Reuben Nhamanilo Kwagilwa, wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Jamii cha Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi - CCRC, kilichopo Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru - TICD.

Mhe. Kwagilwa amesema baada ya kumalizika kwa Bunge la Bajeti ataomba idhini kwa Waziri wa Mazingira kufanya ziara ya kukagua utekelezaji wa upandaji miti katika halmashauri zote 184 nchini ili kujionea hali halisi.

“Bunge hili likiisha nitataka kama serikali kwenda kuangalia hali halisi ya upandaji miti. Kwa kuwa kila mkurugenzi anayeulizwa anasema tumepanda miti milioni 5, milioni 2, lakini ukikagua eneo hilo miti hutaiona kabisa. Maigizo haya ndugu zangu kwenye mazingira ni hatari,” alisema.

Aliongeza kuwa serikali itamchukulia hatua mtu yeyote atakayethibitika kuendeleza shughuli za uharibifu wa mazingira baada ya kupewa taarifa.

Naibu Waziri ameeleza kuwa chanzo kikubwa cha mabadiliko ya tabia nchi ni uharibifu wa vyanzo vya maji, ukataji miti, kilimo kisichozingatia uhifadhi wa ardhi, pamoja na shughuli za viwanda, uvuvi na uchimbaji wa madini usiozingatia utaratibu.

Hali hiyo imesababisha ukame usioelezeka, mvua zisizo na majira, mafuriko, mito kubadilisha mikondo, maziwa kuingia kwenye makazi ya watu, dhoruba na vimbunga.

“Chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira ni  uchafuzi wa vyanzo vya maji, ukataji misitu, kilimo ambacho hakiipi ardhi yetu ikolojia,hali inayochangia ongezeko la  gesi joto kwenye ikolojia ya uso wa dunia na kupelekea mabadiliko ya tabia nchi ambayo tunayaona leo,” alisema Kwagilwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii TICD, Dkt. Bakari George amesema kituo hicho kitashirikiana na jamii na wadau mbalimbali kuandaa sera na kufanya tafiti za kusaidia jamii kuondokana na janga la mabadiliko ya tabia nchi.

Meneja wa CCRC, Dkt. Agnes Kapinga amesema uanzishwaji wa kituo hicho umefuata uchafuzi mkubwa wa mazingira unaopelekea ongezeko la taka kila siku na mifumo kushindwa kustahimili.

“Uwepo wa kituo hicho kwa kushirikiana na taasisi zingine utakujia na majibu ya changamoto mbalimbali zitakazosaidia jamii na taifa kwa ujumla kuwa na ustahimilivu kwa maendeleo endelevu,” alisema Dkt. Kapinga.

Kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM inamtaka kila Mkurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha anapanda miti milioni 1.5 ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.

Naibu waziri wa nchi Ofisi ya Mkuu wa Raisi Muungano na Mazingira Mh.Reuben Nhamanilo Kwagila akizungumza katika hafla hiyo
Naibu waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira akikata Utepe wakati wa Uzinduzi wa kituo Cha Jamii Cha Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi
Mkuu wa chuo Cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD),Dkt.Bakari George akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika chuoni hapo



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...