Na Janeth Raphael- MichuziTv -Dodoma.
Serikali imesema inaendelea kuchukua hatua mahsusi za kupunguza gharama za uzalishaji wa zao la tumbaku ili kuongeza faida kwa wakulima na kuimarisha mchango wa zao hilo katika uchumi wa nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 12, 2026 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Jacqueline Kainja Andrew, aliyetaka kujua ni lini Serikali itaangalia upya gharama za uzalishaji wa tumbaku ili wakulima waweze kunufaika zaidi na kilimo hicho.
Akijibu swali hilo, Silinde amesema Serikali inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima wa tumbaku, ikiwemo ongezeko la bei za pembejeo, gharama kubwa za nishati inayotumika katika ukaushaji wa tumbaku kama kuni na makaa, pamoja na riba kubwa za mikopo kutoka taasisi za kifedha.
Amesema kupitia Bodi ya Tumbaku kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo, tayari Serikali imeanza kufanya tathmini ya kina ya muundo wa gharama za uzalishaji ili kubaini maeneo yanayochangia mzigo mkubwa kwa wakulima na namna ya kupunguza gharama hizo.
“Serikali inaangalia maeneo mbalimbali ikiwemo tozo za vyama vya ushirika, gharama za pembejeo pamoja na masharti ya mikopo inayotolewa kwa wakulima wa tumbaku,” amesema Silinde.
Aidha, amesema Serikali tayari imeanza mazungumzo na benki pamoja na taasisi za kifedha zinazotoa mikopo kwa wakulima wa tumbaku ili kujadili uwezekano wa kupunguza riba na gharama nyingine zinazohusiana na huduma za kifedha.
Kwa mujibu wa Silinde, hatua hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wakulima wa tumbaku wanapata faida stahiki kutokana na jasho lao, huku zikilenga kuongeza tija na kuimarisha uzalishaji wa zao hilo muhimu la biashara nchini.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...