Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma .
Serikali imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuboresha sekta ya usafirishaji wa bodaboda nchini kwa kuagiza halmashauri zote kutenga bajeti maalum kwa ajili ya ujenzi wa vituo na maegesho ya madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda.
Hatua hiyo inalenga kuboresha mazingira ya kazi kwa vijana wanaojishughulisha na huduma za usafirishaji pamoja na kuongeza ufanisi, usalama na utaratibu katika shughuli zao za kila siku.
Akijibu swali la Mbunge wa Bukoba Mjini, Eng. Johnston Johansen Mutasingwa, aliyehoji mpango wa Serikali wa kuwajengea vijana waendesha pikipiki maeneo rasmi ya maegesho, Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema Serikali tayari imeanza kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha sekta hiyo muhimu ya ajira kwa vijana.
Dkt. Dugange amesema Serikali imezielekeza halmashauri zote nchini kuendelea kuwatambua madereva wa bodaboda na kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vyao katika maeneo mbalimbali.
Amesema hadi sasa Serikali imetenga maeneo 662 yenye ukubwa wa mita za mraba 5,859,756.18 katika halmashauri 146 nchini kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo, wakiwemo madereva wa bodaboda.
Aidha, Serikali inaendelea na ujenzi wa ofisi za wafanyabiashara wadogo katika mikoa mbalimbali nchini ili kurahisisha usimamizi, mawasiliano na utekelezaji wa shughuli zao. Ofisi hizo pia zinatarajiwa kuwahusisha madereva wa bodaboda ili kuwapa mazingira bora ya kufanya kazi zao kwa uratibu zaidi.
Kwa mujibu wa Dkt. Dugange, kiasi cha shilingi milioni 260 tayari kimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo katika mikoa 13 nchini.
Ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa utambuzi wa maeneo hayo na utoaji wa namba rasmi, Serikali itaendelea na ujenzi wa maegesho ya bodaboda katika vituo mbalimbali nchini, ikiwemo katika Manispaa ya Bukoba.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia sekta ya usafirishaji, huku ikiweka mazingira rafiki yatakayosaidia shughuli zao kufanyika kwa usalama, utaratibu na ufanisi zaidi.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...