Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Serikali imesema imeendelea kupata mafanikio makubwa katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini kutokana na kuimarika kwa ushirikiano wa ndani na nje ya nchi pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanywa katika sekta ya usalama, intelijensia na udhibiti wa biashara haramu ya dawa hizo.
Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi, katika Mkutano na waandishi wa habari Bungeni Dodoma wakati akiwasilisha Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya nchini kwa mwaka 2025.
Prof. Kabudi amesema Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa kitaifa, kikanda na kimataifa katika kubadilishana taarifa za kiintelijensia, kuendesha operesheni maalum za pamoja pamoja na kujenga uwezo wa taasisi zinazoshughulikia mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Amesema hatua hizo zimeendelea kusaidia kuvunja mitandao ya usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya ambayo imekuwa ikihatarisha usalama wa jamii, afya za wananchi na nguvu kazi ya taifa.
Kwa mujibu wa Prof. Kabudi, mafanikio hayo yanatokana na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuimarisha mifumo ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini kwa kuongeza uwekezaji katika vyombo vya ulinzi, usalama na taasisi za udhibiti.
Amesema Serikali imeendelea kuiwezesha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya pamoja na taasisi nyingine zinazoshiriki katika operesheni za kudhibiti biashara hiyo haramu ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Matokeo haya yanaonyesha namna ambavyo ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali, vyombo vya dola, wataalamu wa afya, wadau wa maendeleo na wananchi unavyoendelea kuzaa matunda katika vita dhidi ya dawa za kulevya,” amesema Prof. Kabudi.
Aidha, amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya hayawezi kufanikiwa bila ushiriki wa wananchi, huku akitoa wito kwa jamii kuendelea kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu vitendo vinavyohusiana na usambazaji, matumizi au biashara ya dawa za kulevya.
Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mikakati ya kinga, elimu kwa umma, tiba na operesheni maalum ili kuhakikisha taifa linaendelea kuwa salama dhidi ya athari za dawa za kulevya ambazo zimekuwa zikichangia mmomonyoko wa maadili, ongezeko la vitendo vya uhalifu pamoja na kuathiri maendeleo ya vijana na jamii kwa ujumla.
Prof. Kabudi pia amewapongeza wananchi kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa vyombo vya usalama na taasisi zinazopambana na dawa za kulevya, akieleza kuwa mchango wa jamii ni msingi muhimu wa ushindi katika mapambano hayo.
Kwa upande wa Kamishina Jenerali Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema tatizo la dawa za kulevya ni suala mtambuka linalohusisha mitandao ya kihalifu iliyopo nchi mbalimballi Duniani, hivyo mapambano dhidi ya tatizo hilo yanahitaj ushirikiano na nguvu za pampja kuanzia ngazi ya Kitaifa, kikanfa bna Kimataifa.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...