Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

SERIKALI Kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) inatekeleza mradi nyumba za makazi kwa watumishi wa Umma vijana ‘Temeke Kota’ jijini Dar es Salaam kwa gharama ya shilingi Bilioni 21 ikiwa ni sehemu ya kutafuta suluhu ya makazi kwa vijana walioajiriwa katika ofisi za Umma na kufuatiwa na miradi itakayowalenga vijana wasio watumishi wa Umma.

Akizungumza leo mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi kwa vijana watumishi wa Umma wa Temeke Kota Jijini Dar es Salaam Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema; mradi huo wa Nyumba za gharama nafuu una nyumba zitakazobeba familia 144 ambapo nyumba 72 ni chumba kimoja na sebule na choo (studio apartment,) na nyumba 72 ni vyumba viwili pamoja na sebule mahususi kwa wenye familia ndogo.

Waziri Ulega amesema,Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan suluhu imejizatiti kutafuta suluhu ya nyumba za makazi kwa gharama nafuu na TBA wamekuwa wakifanya jitihada za kina katika kutatua changamoto hiyo kwa makundi mbalimbali wakiwemo vijana.

“Mradi huu umeanza na vijana wanaoanza kazi ya utumishi wa Umma, na kwa maelekezo ya Serikali TBA wataendelea kujenga nyumba za makazi za vijana kwa ujumla, Mpango wa Rais Samia si kwa vijana watumishi pekee bali kwa kundi lote la vijana hivyo waandishi wa habari, wachuuzi na wafanyabiashara watapata fursa ya kupata makazi bora kwa gharama nafuu.” Amesema.

Kuhusiana na gharama za nyumba hizo Ulega amesema; Bei elekezi ni shilingi laki mbili hadi laki tatu na nusu bei zinazoendana na soko na kuitaka Wakala hiyo kuweka mchakato wa wazi katika upatikanaji wa nyumba hizo bila kuhusisha udalali na walengwa wawe vijana na sifa zote ziwekwe wazi kupitia magazeti na mitandao ili vijana walengwa waweze kupata nyumba hizo za Dkt. Samia.

Aidha ameielekeza TBA kutafuta wabia kutoka sekta binafsi na kushirikiana nao katika utekelezaji wa miradi mbalimbali kama Serikali inavyosisitiza ushirikiano baina ya Taasisi za Umma na sekta binafsi katika nyanja mbalimbali.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Dar es Salaam Arch. Benard Mayemba amesema kuwa, mradi huo wa ghorofa tisa unatekelezwa kwa Ruzuku kutoka Serikalini umegharimu shilingi Bilioni 21 na hadi sasa takribani shilingi Bilioni 10.2 na unategemewa kukamilika Oktoba 2027.

Aidha amesema; Nyumba hizo zimejengwa kisasa na kuwekwa huduma muhimu kama kisima chenye tanki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita laki tano, lift pamoja na eneo maalum la dharura lililotengwa pindi majanga yanapotokea.

Vilevile Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke Uzairu Athuman ameishukuru Serikali kupitia TBA kwa kuelekeza mradi huo katika Manispaa hiyo na kuwataka wanufaika kutunza miradi ya namna hiyo kwa kuitumia kwa kadri ilivyopangwa na Serikali.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...