WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imetoa zawadi ya sh. milioni 500 kwa Timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) kwa kufanikiwa kutinga hatua ya fainali ya mashindano hayo na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania kimataifa.
Dkt. Mwigulu amesema hayo leo (Ijumaa, Mei 29, 2026) ofisini kwake Mlimwa, Dodoma wakati akitoa salamu za pongezi kwa timu hiyo kufuzu hatua ya fainali kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema Rais Samia amewapongeza wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wote wa timu kwa mafanikio hayo makubwa ambayo yameendelea kuandika historia mpya katika sekta ya michezo nchini.
“Mheshimiwa Rais amenielekeza nitoe pongezi hizi kwa vijana wetu wa Serengeti Boys kutokana na mafanikio makubwa ya kutinga fainali na kuiwakilisha vema Tanzania katika mashindano hayo,” amesema Dkt. Mwigulu.
Waziri Mkuu amesema Serikali itatuma ndege maalum kwa ajili ya kuwafuata vijana hao watakapomaliza mashindano hayo ili kurejea nchini pamoja na kombe endapo watafanikiwa kutwaa ubingwa. “Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa ndege kwa ajili ya kuwafuata vijana wetu watakapokuwa wamemaliza mashindano hayo na kurejea nao nyumbani,” amesema.
“Tunaamini huu ni mwanzo tu wa pongezi ambazo Mheshimiwa Rais ameanza kuzitoa. Tunaamini kwamba wakirejea na kombe hilo, kutakuwa na sababu zaidi ya kuwapongeza kwa mafanikio hayo makubwa.”
Waziri Mkuu amemwelekeza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Paul Makonda na wadau wanaohusika, waendelee na uratibu wa wa safari kwa watu watakaokwenda kuwaunga mkono vijana wetu.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amesema endapo Serengeti Boys watatwaa ubingwa, Serikali itawapatia kila mchezaji kiwanja kimoja katika Mji wa Suluhu New City uliopo mkoani Morogoro ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao katika kuitangaza Tanzania kupitia michezo.
Waziri Mkuu pia amewahamasisha Watanzania, taasisi, mashirika na wadau mbalimbali wa michezo kuendelea kutoa msaada na motisha kwa timu hiyo kuelekea mchezo wa fainali.
“Shime shime vijana wetu, inawezekana. Tuleteeni kikombe kile, mleteeni Dkt. Samia Suluhu Hassan kikombe, tuleteeni Watanzania ushindi huo. Kwa kiwango mlichokionesha, tunaamini mna uwezo wa kutwaa ubingwa huo,” amesema.
Sambamba na hilo, Waziri Mkuu amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwa kinara wa maendeleo ya michezo nchini na kuchochea mafanikio yanayoendelea kupatikana katika sekta hiyo.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...