Na Mwandishi Wetu, Siha
Wilaya
ya Siha mkoani Kilimanjaro inatarajiwa kupokea zaidi ya washiriki 800
kutoka ndani na nje ya Tanzania katika mashindano makubwa ya michezo na
utalii yajulikanayo kama West Kili Forest Tour Challenge,
yatakayofanyika Juni 20 hadi 21, 2026 katika ukanda wa msitu wa West
Kilimanjaro.
Mashindano hayo yamezinduliwa rasmi na Mkuu wa
Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka, aliyesema tukio hilo litakuwa
chachu ya kuitangaza Siha kimataifa kupitia utalii wa asili, michezo na
shughuli za kijamii zitakazochochea uchumi wa wananchi.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Timbuka alisema mashindano hayo
yatahusisha mbio za kilomita 5, 10 na 21, pamoja na mashindano ya
baiskeli na pikipiki yatakayopita katika maeneo yenye mandhari ya
kuvutia ya msitu wa West Kilimanjaro.
“Tunatarajia kupokea
washiriki wengi kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania na nje ya nchi. Hii
ni fursa kubwa kwa Siha kuendelea kujitangaza kama kitovu cha utalii wa
michezo na uhifadhi wa mazingira,” alisema Dkt. Timbuka.
Aliongeza
kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika ili kuhakikisha mashindano
hayo yanafanyika kwa mafanikio makubwa huku yakitoa nafasi kwa wananchi
kunufaika kupitia biashara mbalimbali zikiwemo malazi, chakula, usafiri
na huduma nyingine za kijamii.
Kwa mujibu wa waandalizi, kabla ya
siku ya mashindano kutafanyika mkesha maalumu wa burudani
utakaojumuisha shughuli za kijamii, muziki, chakula na vinywaji kwa
washiriki na wadau mbalimbali.
Mashindano hayo yanaungwa mkono na
kampuni ya Mati Super Brands Ltd ambayo imeahidi kushirikiana
kuhakikisha tukio hilo linakuwa la kipekee na lenye mafanikio makubwa.
Akizungumza
kuhusu malengo ya mashindano hayo, Mratibu wa West Kili Forest Tour
Challenge, Bw. Mensier Elly, alisema tukio hilo si la michezo pekee bali
ni jukwaa muhimu la kutangaza vivutio vya utalii vya West Kilimanjaro
na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira kupitia michezo na utalii endelevu.
“Tunataka
kutumia michezo kama njia ya kuhamasisha jamii kuthamini mazingira na
wakati huo huo kuitangaza West Kilimanjaro kwa dunia,” alisema Bw. Elly.
Mashindano
hayo yanatarajiwa kuwa miongoni mwa matukio makubwa ya michezo na
utalii nchini mwaka huu kutokana na ushiriki mkubwa unaotarajiwa pamoja
na mvuto wa kipekee wa mazingira ya West Kilimanjaro.























Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...