Na Janeth Raphael MichuziTv

Serikali imeendelea kuimarisha sekta ya afya nchini kwa kuongeza ajira za watumishi wa kada mbalimbali, hatua inayolenga kupunguza uhaba wa wataalamu katika hospitali, vituo vya afya na zahanati, hususan katika maeneo yenye upungufu mkubwa wa watumishi.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Jafar Seif, amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2025/26 Serikali imeajiri jumla ya watumishi 37,921 wa kada za afya na kuwapangia vituo vya kazi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini.

Dkt. Seif ametoa kauli hiyo bungeni leo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Christina Solomon Mndeme, aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali wa kuongeza watumishi wa afya katika Mkoa wa Tabora ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumzia hali ya Mkoa wa Tabora, Dkt. Seif amesema mahitaji halisi ya wataalamu wa afya ni watumishi 8,121, lakini waliopo sasa ni 3,467 pekee, sawa na asilimia 43 ya mahitaji yote. Hivyo, mkoa huo bado unakabiliwa na upungufu wa watumishi 4,654, sawa na asilimia 57.

Amesema licha ya changamoto hiyo, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kupunguza pengo hilo ambapo kati ya mwaka wa fedha 2024/25 hadi 2025/26, jumla ya watumishi 856 wa kada mbalimbali za afya wameajiriwa na kupangiwa vituo vya kazi katika halmashauri zote za Mkoa wa Tabora.

Aidha, Dkt. Seif amesema halmashauri nane za Mkoa wa Tabora zimeandaa mkakati maalum wa kuongeza nguvu kazi katika sekta ya afya kupitia mapato ya ndani. Kwa mwaka wa fedha 2026/27, halmashauri hizo zimetenga jumla ya shilingi milioni 413.8 kwa ajili ya kuajiri watumishi 87 wa afya kwa mfumo wa mikataba.

Kwa mujibu wa Serikali, hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya karibu na maeneo yao pamoja na kupunguza mzigo wa kazi kwa watumishi waliopo sasa katika vituo vya kutolea huduma.

Serikali imeendelea kusisitiza kuwa itaendelea kuboresha mazingira ya utoaji huduma za afya nchini kwa kuongeza ajira, kuimarisha miundombinu ya afya na kuhakikisha wataalamu wa kutosha wanapatikana katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...