Na Byera Deus-Bukoba.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, imewaomba madiwani kujiunga na mpango wa TAKUKURU Rafiki unaolenga kuzuia rushwa katika jamii kwa njia ya mazungumzo na utatuzi wa kero.

Katika semina fupi iliyoandaliwa na TAKUKURU Mkoa wa Kagera, iliyowakutanisha madiwani, watendaji pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kwa lengo la kujadili uwajibikaji na wajibu wa viongozi katika suala la kuzuia rushwa, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, Leonard Swai, alisema kuwa mpango wa TAKUKURU Rafiki unalenga kuokoa miradi na kumaliza rushwa kwa njia ya mazungumzo.

Alisema changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni malalamiko juu ya miradi, ambapo malalamiko hayo hutolewa baada ya mradi kufika hatua za mwisho, wakati kinachotakiwa ni kumaliza tatizo kabla ya mradi kutekelezwa hadi mwisho. Amewataka madiwani kushiriki katika mpango huo ili kuokoa miradi ya maendeleo inayogusa wananchi wao.

“Tusisubiri mpaka watu wakamatwe kwenda mahakamani, huko kuna sheria ngumu, ni vizuri tukawa timu tukashauriana, na mara nyingi wananchi mpaka kufika kwetu wanakuwa wamepitia kero ambazo hazina majibu. Ni vizuri madiwani, wakuu wa idara pamoja na watendaji wakishirikiana vizuri sana wataepusha changamoto nyingi na hakuna mradi ambao utapotea.”

Aidha, alisema wajibu mwingine wa madiwani, pamoja na kusimamia jamii, ni kuendelea kuwasimamia watendaji pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ili kuongeza ufanisi wa mapato ya ndani na kuiwezesha halmashauri kujiendesha kwa ufanisi zaidi, pia aliwataka watendaji kuacha tabia za kukaanga fedha wanazokusanya kwenye vyanzo vya mapato ili wasipelekwe mahakamani.

Kwa upande wao, baadhi ya madiwani walieleza kuwa semina hiyo imewapa uelewa mpana kuhusu masuala ya rushwa na kudai kuwa wanapaswa kushirikishwa katika miradi ya maendeleo ili waweze kuibua vitendo vya rushwa mapema kwa njia rafiki na kuwezesha miradi kukamilika kwa wakati.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Fatina Hussein Laay, alisema kuwa mpango wa TAKUKURU Rafiki ni mpango mzuri kwani unalenga kufanya uchambuzi wa makosa gani yanapaswa kupelekwa mahakamani au kujadiliwa kwa njia rafiki, ameishukuru TAKUKURU kwa mafunzo kwa madiwani kwani wao ndio wasimamizi wakubwa wa maendeleo ya kata.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...