Na. Aron Msigwa - Monduli, Arusha

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limewataka washiriki wa Tanzania wanaokwenda kushiriki zoezi la pamoja la kijeshi la Ushirikiano Imara 2026 nchini Kenya kuzingatia nidhamu, uzalendo na weledi ili kuendelea kuiwakilisha vyema Tanzania katika jukwaa la kimataifa.

Kauli hiyo imetolewa Mei 9, 2026 na Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu , Meja Jenerali Fadhili Omary Nondo, wakati wa hafla ya kukabidhi Bendera ya Taifa kwa kikosi kitakachoshiriki zoezi hilo, iliyofanyika katika uwanja wa Brigedi Mbuni 303, Kundi la Vikosi, wilayani Monduli mkoani Arusha.

Meja Jenerali Nondo amesema washiriki wanapaswa kufuata maelekezo yote ya viongozi wao na kutumia mafunzo waliyopewa kama msingi wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.

Ameeleza kuwa zoezi hilo la 14 la pamoja la vituo vya uamrishaji vya kijeshi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) lina lengo la kuongeza uwezo wa vikosi vya nchi wanachama kukabiliana na changamoto za usalama, kudumisha amani na kuimarisha ushirikiano wa kijeshi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Tunatarajia washiriki wote kutoka Tanzania mtaonesha uwezo mkubwa, nidhamu na uzalendo ili kuendelea kuipa heshima nchi yetu. Ni matumaini ya Mkuu wa Majeshi pamoja na Wakuu wetu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuwa washiriki wote kutoka Tanzania mtatekeleza na kutimiza lengo kuu la zoezi la ushirikiano imara 2026 na kujenga uwezo katika kukabiliana na changamoto ambazo Jumuiya imekubaliana kuzitatua kwa pamoja ” amesema Meja Jenerali Nondo.

Aidha, amesema mazoezi hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uwezo wa vikosi vya ulinzi na usalama kukabiliana na majanga,uharamia, migogoro na matishio mbalimbali ya kiusalama, sambamba na kukuza uhusiano mzuri miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikundi cha Tanzania kinachokwenda nchini Kenya ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa zoezi hilo kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Brigedia Jenerali Maneno Almasi Mabakila, amesema zoezi hilo litafanyika nchini Kenya kuanzia Mei 13 hadi 28, 2026 likihusisha washiriki 341 kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Somalia.

Amesema Tanzania itawakilishwa na washiriki 69 wakiwemo maafisa na askari wa JWTZ 42,  washiriki kutoka Jeshi la Polisi 9 na watumishi 18 kutoka taasisi zinazoshughulikia masuala kiraia.

Brigedia Jenerali Mabakila amesema washiriki hao tayari wamepata mafunzo maalumu ya pamoja ikiwemo operesheni za kulinda amani, kupambana na ugaidi, kudhibiti majanga, kupambana na uharamia pamoja na mafunzo ya vituo vya uamrishaji vya kijeshi.

Amesisitiza kuwa kikosi hicho kiko tayari kushiriki zoezi hilo kwa ufanisi mkubwa na kuendelea kudhihirisha uwezo wa Tanzania katika masuala ya ulinzi na usalama wa kikanda.










Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...