MKUU wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni, ameisisitiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilayani humo kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato pamoja na kuhamasisha matumizi ya mashine za kielektroniki za utoaji risiti (EFD) ili kulinda mapato ya serikali yasipotee.
Hayo ameyazungumza jana katika kikao cha Kamati ya Ushauri wa Kodi ya Wilaya ya Same ambapo alisema licha ya wilaya hiyo kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato na kuvuka lengo lililowekwa, bado kuna umuhimu wa kuongeza jitihada katika kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuimarisha matumizi ya mashine za EFD kwa wafanyabiashara wote.
“Tumefanya vizuri na kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato lililowekwa, lakini bado tuna wajibu wa kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuendelea kuhamasisha matumizi ya mashine za EFD ili kuzuia upotevu wa fedha za serikali,” alisema Kasilda.
Aidha, aliwataka maafisa wa TRA kuwa karibu zaidi na wafanyabiashara pamoja na wananchi kwa kuwapa elimu ya mara kwa mara kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari na kuwasisitiza wananchi kudai risiti kila wanaponunua bidhaa au huduma mbalimbali.
Kwa upande wake Afisa wa TRA Wilaya ya Same, Angela Mwakaje, alisema kuwa taasisi hiyo imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 7.7 katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, huku lengo lililowekwa likiwa ni shilingi bilioni 7.2.
Alieleza kuwa mafanikio hayo yameiwezesha TRA Same kufikia asilimia 107.5 ya makusanyo na hivyo kuvuka lengo lililopangwa.
Angela alisema mafanikio hayo yametokana na juhudi za kutoa elimu kwa walipakodi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari pamoja na kuhamasisha wananchi kudai risiti kila wanaponunua bidhaa mbalimbali.
Kikao hicho cha Kamati ya Ushauri wa Kodi ni cha kisheria na hufanyika mara mbili kwa mwaka kwa lengo la kujadili mwenendo wa ukusanyaji wa mapato wilayani humo pamoja na kupendekeza mikakati bora ya kuhakikisha malengo ya mapato yanafikiwa.




.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...