NA FARIDA MANGUBE MOROGORO

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeandika rekodi ya kipekee nchini baada ya kutangaza kufanikiwa kupata Hati Safi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka 20 mfululizo.

Rekodi hiyo ya kihistoria ya uwajibikaji na usimamizi bora wa fedha imetangazwa wakati wa Mahafali ya 47 ya chuo hicho yaliyofanyika katika Kampasi Kuu ya Edward Moringe.

Mbali na rekodi hiyo ya CAG, SUA imeendeleza ubabe wake wa kifedha baada ya kutunukiwa tuzo ya kuwa taasisi ya juu ya elimu inayoongoza kwa uandaaji bora wa hesabu nchini na Bodi ya NBAA kwa miaka mitatu mfululizo.

Mafanikio haya makubwa yameongeza chachu ya furaha katika mahafali hayo yaliyoshuhudia jumla ya wahitimu 877 wakitunukiwa shahada za Uzamivu, Uzamili, Shahada za Kwanza, Stashahada za juu, Stashahada na Astashahada mbalimbali chini ya uongozi wa Mkuu wa Chuo, Jaji Joseph Sinde Warioba.

Akiwasilisha ripoti hiyo ya mafanikio ya fedha na utawala bora mbele ya hadhara, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Raphael Chibunda amesema

"Tumendelea kuimarisha nidhamu katika majukumu ya chuo, na hatua hiyo imekiwezesha chuo chetu kupata hati safi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Hii inaendeleza rekodi yetu ya hati safi kwa dhihirisho la miaka 20 mfululizo."

Profesa Chibunda amebainisha kuwa wahitimu hao 877 wanatoka katika programu 83 za masomo kati yao, wanaume ni 517 na wanawake ni 360.

Uchambuzi wa kitaaluma unaonyesha kuwa wahitimu wa Shahada za Kwanza (Bachelor) walikuwa 698, Shahada za Umahiri (Masters) 132, Shahada za Uzamivu 19, Stashahada 141, na Astashahada 23.

Katika hatua nyingine ya maendeleo, Profesa Chibunda ametangaza kuwa chuo kipo hatua za mwisho kuzindua kituo chake rasmi cha runinga cha SUA TV, ambacho kitakuwa nyanja ya kimkakati ya kusambaza teknolojia za kisasa za kilimo, mifugo, na uvuvi kwa jamii.

Pia, amejivunia vijana wa SUA Innovation Hub kupitia timu za Snackers Square na Eco Mushroom kwa kushika nafasi ya kwanza kitaifa kwenye mashindano ya Youth Ignite Student Founders Fellowship, akisisitiza kuwa chuo kimebobea katika kuwajenga wanafunzi kiuandishi na kiubunifu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Ndugu Andrew Masawe, akizungumza kuhusu dira na majukumu ya Baraza katika kusimamia chuo, ameeleza kuwa Baraza limeendelea kuboresha sura na utendaji wa Chuo kwa ujumla.

"Baraza limeendelea kwa kiasi kikubwa kutekeleza mambo mengi makubwa yanayolenga kuboresha sura na utendaji wa chuo kwa ujumla Pia, Baraza limeidhinisha nyaraka muhimu za kimkakati ikiwemo miongozo ya ukuzaji wa machapisho ya Maktaba ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2025."Amesema Massawe.

Masawe ametaja pia kuanzishwa kwa Kituo kipya cha Sera na Mafunzo ya Kimkakati (SUA Center for Policy and Strategic Studies) ili kuishauri serikali katika sera zenye tija, huku akitoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi bilioni 20.7 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Kampasi ya Mizengo Pinda mkoani Katavi.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...