Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma 

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeendelea kuonesha dhamira yake ya kupunguza pengo la kidijitali nchini kwa kutekeleza miradi mbalimbali inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano, intaneti na kuwajengea uwezo wananchi, hususan wasichana na vijana, katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Hayo yameelezwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Albert Richard, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya mfuko huo katika semina iliyowakutanisha waandishi wa habari na wahariri jijini Dodoma.

Akizungumza katika semina hiyo, Mhandisi Richard amesema UCSAF imefanikiwa kuwajengea uwezo wanafunzi 1,300 wa kike kutoka shule za sekondari za umma kupitia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Msichana na TEHAMA (Girls in ICT Day), ambayo huadhimishwa kila mwaka mwezi Aprili.

Amesema kupitia maadhimisho hayo, wanafunzi hupatiwa mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya TEHAMA, ubunifu wa kidijitali pamoja na fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya teknolojia, hatua inayolenga kuwahamasisha wasichana kujikita katika masomo na taaluma zinazohusiana na sayansi, teknolojia na mawasiliano.

“Lengo letu ni kupunguza pengo la ushiriki lililopo kati ya wasichana na wavulana katika sekta ya TEHAMA na kuhakikisha wasichana wanapata nafasi sawa katika ulimwengu wa kidijitali,” amesema Mhandisi Richard.

Amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, UCSAF kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ilifanikiwa kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa jumla ya wasichana 440, wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi, sekondari, vyuo, elimu ya awali pamoja na wenye ulemavu.

Mafunzo hayo yalitolewa katika vituo vya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya na Zanzibar, huku yakilenga kuongeza uelewa wa matumizi ya teknolojia na kuwapa washiriki ujasiri wa kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.

Mbali na uwezeshaji wa vijana, UCSAF pia inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kutoa huduma za bure za intaneti katika maeneo ya wazi yenye matumizi makubwa ya wananchi, ikiwa ni sehemu ya kuongeza upatikanaji wa huduma za kidijitali kwa urahisi zaidi.

Kupitia mradi huo, vituo 17 vya intaneti ya bure vimeanzishwa katika Viwanja vya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba jijini Dar es Salaam. Aidha, huduma hiyo imefikishwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Nyerere Square na Chuo cha Informatics CIVE jijini Dodoma, Soko la Nyamagana jijini Mwanza, Kiembesamaki Zanzibar, Soko la Tabora pamoja na Lungemba Training College iliyopo Mafinga.

Kwa mujibu wa Mhandisi Richard, katika mwaka wa fedha 2024/2025 UCSAF pia ilitekeleza mradi wa intaneti ya bure katika vituo 25 vya mabasi ya mwendokasi (BRT-DART) kwa gharama ya shilingi milioni 500.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026, utekelezaji wa mradi huo unaendelea katika maeneo 60 ya Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwa ni jitihada za kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma za intaneti kwa urahisi na gharama nafuu.

Katika hatua nyingine, UCSAF inaendelea kutekeleza mradi wa kuunganisha ofisi za halmashauri na mkongo wa taifa wa mawasiliano kwa njia ya faiba ili kuboresha huduma za intaneti katika taasisi za umma.

Mhandisi Richard amesema tayari utambuzi wa maeneo 10 umekamilika, huku mchakato wa manunuzi ukiendelea ili kumpata mkandarasi atakayetekeleza kazi ya kuunganisha huduma hizo pamoja na kujenga miundombinu ya kufikisha faiba katika maeneo husika.

Sambamba na hilo, UCSAF inaendelea na mradi wa kuongeza uwezo wa minara 62 ya mawasiliano kutoka teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G, hatua inayolenga kuboresha huduma za mawasiliano na intaneti katika maeneo ya vijijini.

Amesema kati ya minara hiyo, minara 37 inatekelezwa na kampuni ya Vodacom ambapo tayari imekamilika na imeanza kutoa huduma ya intaneti yenye kasi, huku minara 25 inayotekelezwa na TTCL ikiwa katika hatua za awali za manunuzi.

Kwa mujibu wa UCSAF, utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kuongeza uwezo wa wananchi kupata huduma bora za mawasiliano, kukuza matumizi ya huduma za kidijitali na kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi kupitia teknolojia.

Aidha, miradi hiyo inatarajiwa kusaidia kuboresha huduma muhimu kama elimu mtandao, afya mtandao, biashara mtandao pamoja na huduma za kifedha kupitia simu za mkononi, hasa kwa wananchi wa maeneo ya vijijini na yasiyokuwa na huduma bora za mawasiliano.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...