Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Zauda Mohamed, ameongoza mafunzo maalum kwa walimu wa vyuo vya udereva jijini Arusha, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha ubora wa mafunzo ya udereva na kuongeza usalama barabarani Pamoja na Kuimarisha matumizi ya Tehama katika Usimamizi wa vyuo hivyo.
Mafunzo hayo yanaendelea kutolewa katika Chuo cha Ufundi Arusha (Arusha Technical College - Arusha Tech), ambapo walimu hao wanapatiwa ujuzi na mbinu za kisasa zitakazowawezesha kuandaa madereva wenye sifa, weledi na uelewa unaokidhi mahitaji ya sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani za sasa.
Akizungumza baada ya mafunzo hayo, ACP Zauda Mohamed amesema lengo la Kikosi cha Usalama Barabarani ni kuhakikisha walimu wa vyuo vya udereva wanakuwa na uwezo wa kuzalisha madereva wenye viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.
“Tunataka kuona madereva wanaopata mafunzo kutoka kwa walimu hawa wanakuwa na sifa stahiki na kuzingatia sheria za usalama barabarani. Hii itasaidia kupunguza ajali za barabarani na hatimaye kuokoa maisha ya wananchi,” amesema ACP Zauda.
Ameongeza kuwa kikosi hicho kinaendelea kuweka mkazo katika utoaji wa elimu na mafunzo kwa wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji ili kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua kwa kiwango kikubwa, na ikiwezekana kutokomezwa kabisa.
Pia amewataka walimu hao kuendelea kuboresha mbinu za ufundishaji na kuzingatia mabadiliko ya teknolojia pamoja na mahitaji ya soko la ajira, akibainisha kuwa kwa sasa mahitaji ya madereva wenye taaluma na ujuzi wa kutosha yanaongezeka ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wao, baadhi ya walimu wa vyuo vya udereva waliohudhuria mafunzo hayo wamelishukuru Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha kwa kuendelea kuwawezesha kitaaluma mara kwa mara.
Wamesema mafunzo hayo yanawajengea uwezo wa kufundisha kwa viwango vya juu zaidi na kuwasaidia kuzalisha madereva wenye umahiri unaokidhi vigezo vya kitaifa na kimataifa.



.jpeg)
.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...