Serikali imesema bado kuna watu wanaopinga mfumo wa stakabadhi za ghala kwa sababu zamani walikuwa wakinufaika kwa kuwanyonya wakulima kupitia biashara ya mazao, huku ikisisitiza kuwa mfumo huo umewekwa kwa lengo la kuhakikisha wakulima wanapata bei nzuri na faida halali ya mazao yao.
Hayo yameelezwa Mei 17, 2026 na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, wakati akifungua uzinduzi wa maonesho ya maadhimisho ya miaka 20 ya mfumo wa stakabadhi za ghala yaliyofanyika Jijini Dodoma.
Ameeleza kuwa mfumo huo umeendelea kuwa mkombozi kwa wakulima kwa kuwawezesha kuhifadhi mazao yao katika mazingira mazuri na kupata bei yenye ushindani tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo baadhi ya wafanyabiashara walinunua mazao ya wakulima kwa bei ya chini iliyowapa hasara wakulima hao.
Londo amesema Serikali imeweka mazingira rafiki na wezeshi kupitia mfumo huo ili kuwasaidia wakulima kunufaika zaidi na mazao yao, huku baadhi ya watu wanaoupinga wakitaka kurejesha mazingira ya zamani yaliyokuwa yakiwanyima wakulima haki zao.
Aidha amesema kuwa, kilimo kinaendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa, hivyo Wizara ya Viwanda na Biashara imepewa jukumu la kuhakikisha wakulima wananufaika na mazao yao pamoja na kuongeza ushindani katika biashara ya mazao nchini.
Pia amesema katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea kuimarisha mfumo wa stakabadhi za ghala ili kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo na kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ya kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa juu.
Amesema kuwa ushiriki wa sekta binafsi unatarajiwa kuchangia asilimia 70 kwenye ukuaji wa uchumi, huku akieleza kuwa ushirikiano wa taasisi zilizo chini ya Wizara za Viwanda na Biashara, Kilimo pamoja na Fedha umeendelea kuimarisha mfumo huo.
Hata hivyo, amesema Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala imeendelea kuwa mshirika muhimu katika kuimarisha ushindani wa biashara ya mazao nchini kwa kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za ununuzi, huku ikiwawezesha wakulima kupata masoko ya uhakika na bei nzuri za mazao yao kupitia mfumo unaolenga kuongeza uwazi, tija na manufaa kwa wakulima.
Kwa upande wake, Witness Temba Afisa udhibiti ubora kutoka Bodi ya Usimamizi wa stakabadhi za Ghala, amesema katika kipindi cha miaka 20, Bodi hiyo imeendelea kutoa leseni kwa wadau mbalimbali wa biashara ya mazao na kuboresha uhifadhi wa mazao, jambo lililosaidia kupunguza upotevu wa mazao na kukuza uchumi wa wakulima.
Aidha, washiriki wa maonesho hayo wametakiwa kutumia fursa hiyo kubadilishana uzoefu na mawazo yatakayochangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 pamoja na kukuza uchumi wa Taifa kupitia sekta ya kilimo na biashara.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...