Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele, amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi wa Uchumi na Uzalishaji, Madaktari wa Mifugo na Uvuvi wa Mikoa, Maafisa Uvuvi wa Mikoa na Wakuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji, uadilifu na uzalendo mkubwa ili kuleta mabadiliko katika Sekta hizo mbili na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza kwa Niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, leo Mei 25, 2026 Jijini Dodoma katika Kikao kazi kilichojumuisha Wataalam mbalimbali wa Taasisi za Serikali wa Sekta hizo mbili za Mifugo na Uvuvi, Dkt. Madele amesema lengo la Kikao hicho ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji na usimamizi wa vipaumbele vya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027, na kusaidia kutoa mwelekeo na Mikakati ya pamoja ya utekelezaji wa vipaumbele hivyo.

"Ni matumaini yangu kuwa mtatumia jukwaa hili kujadili kwa kina mafanikio na changamoto katika utekelezaji wa majukumu ya Sekta pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizo, na kikao hiki kiwe fursa ya kujenga uelewa wa pamoja katika masuala ya Sekta, kubadilishana uzoefu pamoja na kujadili namna bora ya kuimarisha utekelezaji wa shughuli za Sekta kwa uadilifu na weledi." amesema Dkt. Madele

Aidha, Dkt. Madele amewataka Watendaji hao kujadili kwa kina na kwa undani suala la Uvuvi haramu na kuja na Mikakati ya kudhibiti Uvuvi haramu ambayo haitatumia gharama kubwa sambamba kuhamasisha usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi, na jinsi ya kutekeleza Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo inayolenga kudhibiti magonjwa ya mifugo, ili kuongeza uzalishaji na kuwezesha upatikanaji wa masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.

Vilevile, Dkt. Madele amesema kuwa Wizara kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, imeendelea kuandaa Mipango ya matumizi bora ya ardhi iliyowezesha kutenga hekta 196,324.25 za maeneo ya malisho, na hii ni moja ya njia Bora itakayosaidia kupunguza migogoro ya ardhi kwani wafugaji wataweza kupanda Malisho kwa ajili ya Mifugo yao.

Pia, Dkt. Madele ameweka wazi jinsi Wizara inavyoendelea kuweka Mazingira wezeshi yatakayochangia kurahisisha Utendaji kazi wa Wataalam hao wa Sekta zote mbili na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele vilivyobainishwa katika Hotuba ya Bajeti ya mwaka 2026/2027.

Dkt. Madele ameelezea juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Waziri wake Mheshimiwa Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, katika kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha Sekta hizo nchini ili kuongeza uzalishaji, masoko na thamani ya mazao ya mifugo na uvuvi, hatua ambazo ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa mbari bora za mifugo na viumbemaji, kuimarisha upatikanaji wa mbegu za malisho, vyakula vya mifugo na samaki, na upatikanaji wa maji, kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na uvuvi, kukuza masoko na biashara ya mazao ya mifugo na uvuvi, na kuimarisha afya ya mifugo, viumbemaji na mifumo ya utambuzi wa Mifugo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Nchini (DRTE), Ndg. Samwel Mdachi amesema Kikao hicho kinatoa fursa kwa Watendaji wa Sekta za Mifugo na Uvuvi, ya kujadili utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Wizara ikiwemo uwezeshaji wa vijana kupitia mikopo yenye masharti nafuu, uzalishaji wa malisho, uandaaji na usimamizi wa Sera, Miongozo na Mikakati ya Sekta katika udhibiti wa magonjwa ya mifugo, ukusanyaji na usimamizi wa takwimu na maduhuli, utekelezaji wa Miradi ya maendeleo, pamoja masuala ya Ukuzaji viumbe maji.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...