Na Janeth Raphael MichuziTv Bungeni - Dodoma

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Leonard Akwilapo amesema Wizara hiyo imejipanga kuanzisha mabaraza mapya 18 ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya katika mwaka wa fedha 2026/27 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha huduma za utatuzi wa migogoro ya ardhi zinapatikana katika wilaya zote 139 nchini.

Waziri Dkt. Akwilapo ameyasema hayo bungeni leo  wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2026/27, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa haki kwa wananchi pamoja na kuharakisha usikilizwaji wa mashauri ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema pamoja na kuanzishwa kwa mabaraza hayo mapya, Wizara itaendelea kushughulikia mashauri 10,782 ya ardhi yaliyobaki kutoka kipindi kilichopita sambamba na mashauri mapya yatakayofunguliwa katika mwaka ujao wa fedha.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuboresha mifumo ya utoaji haki katika sekta ya ardhi kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya wananchi ya kupata suluhisho la migogoro ya ardhi kwa wakati na kwa haki.

“Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya haki karibu yao na kwa wakati. Kuanzishwa kwa mabaraza haya mapya kutasaidia kupunguza mlundikano wa mashauri na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa migogoro ya ardhi,” alisema Dkt. Akwilapo.

Katika hotuba yake, Waziri huyo pia aliwataka wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kuendelea kuzingatia misingi ya weledi, uadilifu na haki wanaposhughulikia mashauri yanayowasilishwa mbele yao ili kuongeza imani ya wananchi kwa taasisi hizo.

Amesisitiza kuwa mwenendo wa utoaji haki katika mashauri ya ardhi unapaswa kuzingatia sheria, uwazi na usawa bila upendeleo, akieleza kuwa wananchi wengi hutegemea mabaraza hayo kama sehemu muhimu ya kupata haki zao katika migogoro ya ardhi na makazi.

Aidha, Dkt. Akwilapo amesema Wizara imeendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shughuli zake mbalimbali kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Alieleza kuwa matumizi ya mifumo hiyo yamechangia kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma za ardhi pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kupitia mifumo ya kidijitali.

Waziri huyo alibainisha kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika maboresho ya mifumo ya TEHAMA ili kuhakikisha huduma za sekta ya ardhi zinapatikana kwa haraka, kwa urahisi na kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi katika maeneo yote nchini.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha sekta ya ardhi nchini, kupunguza migogoro ya ardhi na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali hiyo muhimu kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...