Na Farida Mangube, Morogoro
Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara imeahidi kuendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha vijana nchini kukuza vipaji vyao vya ubunifu pamoja na shughuli za ujasiriamali, hatua inayolenga kuongeza ajira, kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na kuchochea maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Aristides Mbwasi, amesema hayo wakati alipomwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Judith Kapinga, katika hafla ya kufunga maadhimisho ya Siku ya Mzumbe sambamba na Kambi ya Ujasiriamali iliyofanyika katika Chuo Kikuu Mzumbe.
Mbwasi amesema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na vijana katika kukuza uchumi kupitia bunifu mbalimbali wanazoziibua kila siku, hivyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za elimu ya juu pamoja na wadau wengine wa maendeleo ili kuhakikisha ubunifu huo unakuwa na tija kwa jamii na taifa.
Amesema kuwa katika kipindi hiki ambacho dunia imejaa ushindani mkubwa wa kiuchumi na kiteknolojia, vijana wanapaswa kupewa nafasi pana zaidi ya kuonyesha uwezo wao kwa kuanzisha biashara, viwanda vidogo na miradi ya ubunifu itakayoweza kuzalisha ajira na kuongeza kipato.
“Serikali inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kukuza uchumi wa viwanda na biashara nchini. Hivyo, tunatambua kuwa vijana wabunifu ni nguzo muhimu katika safari hii ya maendeleo. Ndiyo maana tunaendelea kushirikiana na vyuo vikuu pamoja na taasisi mbalimbali ili kuhakikisha vijana wanapata elimu, maarifa na fursa zitakazowasaidia kufikia ndoto zao,” amesema Mbwasi.
Aidha, amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, ikiwemo Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) pamoja na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), kuendelea kuwa karibu zaidi na vijana wabunifu na wajasiriamali chipukizi ili kuwasaidia kurasimisha biashara zao, kupata elimu ya biashara na kuendeleza bunifu zao.
Mbwasi amesema ushirikiano huo utasaidia kuongeza thamani ya bunifu zinazobuniwa na vijana, kuwajengea uwezo wa kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi, pamoja na kuongeza mchango wao katika pato la taifa.
“Tunataka kuona vijana wengi zaidi wakitoka kwenye mawazo ya ubunifu na kuyageuza kuwa biashara rasmi zinazoweza kuajiri watu wengine na kuongeza mapato ya Serikali kupitia shughuli za uzalishaji na biashara,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, amewapongeza viongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuendelea kuandaa programu na majukwaa yanayowapa wanafunzi na vijana nafasi ya kujifunza kuhusu ujasiriamali, ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Allen Mushi, amesema chuo hicho kimeendelea kuweka mazingira yanayowasaidia wanafunzi kubadili maarifa wanayopata darasani kuwa miradi halisi ya biashara na ubunifu yenye manufaa kwa jamii.
Profesa Mushi amesema kupitia Kitengo cha Ubunifu, Ujasiriamali na Mahusiano ya Kitasnia, chuo hicho kimefanikiwa kuibua na kusaidia kuanzishwa kwa zaidi ya makampuni 100 yanayofanya shughuli zake katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema mafanikio hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana, kwani baadhi ya wahitimu wamefanikiwa kujiajiri wenyewe huku wengine wakitoa ajira kwa Watanzania wenzao kupitia biashara na kampuni walizoanzisha.
“Tunajivunia kuona vijana wetu wakitumia elimu wanayoipata chuoni kuanzisha miradi yenye tija kwa jamii. Hii ni ishara kuwa elimu ya juu inaweza kuwa nyenzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya uchumi na kuibua kizazi cha vijana wabunifu na wenye uwezo wa kujitegemea,” amesema Profesa Mushi.
Naye Meneja wa Kitengo cha Ubunifu, Ujasiriamali na Mahusiano ya Kitasnia chuo kikuu Mzumbe amesema Mzumbe imeendelea kushirikiana na sekta binafsi, taasisi za fedha na wadau wa maendeleo ili kuwajengea vijana uwezo wa kubuni biashara endelevu zinazoweza kukua na kushindana katika soko.
Ameeleza kuwa kupitia kambi mbalimbali za ujasiriamali zinazoandaliwa na chuo hicho, vijana wamekuwa wakipata mafunzo ya vitendo kuhusu usimamizi wa biashara, matumizi ya teknolojia, ubunifu wa bidhaa pamoja na mbinu za kutafuta masoko.
Maadhimisho ya Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali yamewakutanisha wanafunzi, wadau wa elimu, taasisi za Serikali, sekta binafsi pamoja na wabunifu mbalimbali kwa lengo la kujadili namna bora ya kutumia ubunifu na ujasiriamali kama nyenzo ya maendeleo ya kiuchumi nchini.











Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...