Na Hassan Kimweri, WAF - Kagera
Tanzania imeendelea kuimarisha udhibiti dhidi ya ugonjwa wa Ebola kwa kushirikiana na nchi jirani ikiwemo Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi na Kenya kupitia ushirikiano wa kikanda ili kudhibiti kusambaa kwa maambukizi ya Ebola.
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema Hayo leo Mei 30, 2026 akiwa katika ziara mkoani Kagera kwa lengo la kukagua udhibiti na utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo mipakani pamoja na vituo vya afya vya kutolea huduma za dharula akiambatana na timu kutoka Wizara ya Afya, OWM- TAMISEMI na Mkoa wa Kagera.
"Zaidi ya wasafiri elfu 75,000 wamefanyiwa uchunguzi katika mipaka mbalimbali nchini tangu kuongezeka kwa tahadhari za Ebola, huku takribani watu 45,000 wakifanyiwa tathmini ya kina zaidi kutokana na kuhisiwa lakini hakuna aliyebainika na ugonjwa wa Ebola," amesema Dkt. Magembe
Amesema, Serikali imeweka mifumo ya ufuatiliaji katika mipaka yote ya nchi ikiwemo mipaka ya nchi kavu, viwanja vya ndege, bandari na maeneo mengine ya kuvukia, ambapo wasafiri wote wanaingia nchini hupimwa na kufanyiwa uchunguzi wa afya.
Aidha, Dkt. Magembe amesema kuwa wahisiwa hao walitambuliwa kwa kuzingatia vigezo vya kitaalamu vya uchunguzi wa Ebola vya kitaifa na kimataifa kama inavyoelekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ikiwemo historia ya kusafiri kutoka maeneo yenye maambukizi, kuwasiliana na watu wenye dalili zinazofanana na Ebola au kuwa na baadhi ya dalili zinazohusishwa na ugonjwa huo.
“Tumefanya vipimo na uchunguzi kwa watu wote waliotiliwa shaka, lakini hadi sasa hakuna hata mtu mmoja aliyebainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola nchini Tanzania,” amesema Dkt. Magembe.
Amefafanua kuwa dalili za Ebola zinaweza kufanana na magonjwa mengine , hivyo amewataka wataalamu wa afya katika vituo vya kutolea huduma kuendelea kuwahoji na kuwachunguza wagonjwa wote wenye dalili zinazoweza kuashiria magonjwa ya mlipuko huku wakichukua tahadhari zote muhimu kujikinga ili wasipate maambukizi.
Mwisho, Dkt. Magembe amewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kupitia namba ya dharura 199 , ofisi za serikali za vijiji na mitaa na vituo vya afya vilivyo karibu nao pindi wanapobaini mtu mwenye dalili zinazotia shaka, akisisitiza kuwa watumishi wa afya wanaendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa salama dhidi ya ugonjwa wa Ebola.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa huduma za Kinga Wizara ya Afya Dkt. Otilia Gowelle amesema mwananchi yeyote anaefika katika kituo cha kutolea huduma anapata elimu sahihi ya namna ya kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo kutoa elimu kupitia TV, vipeperushi pamoja na watoa huduma za afya.











Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...