Benki ya Absa Tanzania jana imeandaa semina ya ngazi ya juu kwa wawekezaji wa taasisi, ikiwakutanisha wadau muhimu kutoka kampuni za bima, taasisi za fedha ndogo, wasimamizi wa mifuko ya uwekezaji, madalali wa masoko ya fedha na mifuko ya hifadhi ya jamii kujadili mwelekeo wa uchumi wa Tanzania pamoja na mwenendo unaojitokeza katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Warsha hiyo, iliyowavutia wawakilishi kutoka taasisi zisizo za kibenki za huduma za kifedha, wadhibiti wa sekta na viongozi wa tasnia mbalimbali, ililenga kuwapatia wawekezaji maarifa ya vitendo kuhusu namna ya kukabiliana na mazingira ya uchumi wa dunia yanayozidi kuwa magumu kutokana na mabadiliko ya viwango vya riba, kuyumba kwa thamani za sarafu pamoja na hali ya kutokuwa na uhakika wa kisiasa na kiuchumi duniani.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha za Kigeni wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Irene Rwegalulira, alisisitiza umuhimu wa maandalizi na kufanya maamuzi ya kimkakati katika mazingira ya masoko yanayobadilika kwa kasi.

“Mafanikio katika mazingira ya sasa hayategemei uwezo wa kutabiri kila mabadiliko ya soko. Kinachohitajika ni kuwa tayari, kulindwa na kuwa katika nafasi nzuri wakati mabadiliko yanapotokea,” alisema.

Bi. Irene alisema kuwa licha ya mabadiliko yanayoendelea katika uchumi wa dunia na wa ndani ya nchi, bado kuna fursa kwa wawekezaji watakaokuwa na taarifa sahihi pamoja na mikakati madhubuti ya usimamizi wa hatari.

Alisisitiza tena dhamira ya Absa ya kuendelea kuwasaidia wateja wake wa taasisi kupitia utaalamu wa masoko, suluhisho bunifu za kifedha na ushauri wa kimkakati.

“Jukumu letu kama mshirika wenu katika Masoko ya Kimataifa ni kuwasaidia kukabiliana na hali ya kutokuwa na uhakika, kusimamia hatari kwa ufanisi na kutumia fursa zilizopo kwa kujiamini na kwa usahihi,” alisema.

Warsha hiyo iliandaliwa kwa ushirikiano na Shirika la Tanzania Reinsurance Corporation (Tan Re), ambapo mchango wake katika kuimarisha sekta ya bima na huduma za kifedha nchini kupitia usimamizi madhubuti wa hatari ulitambuliwa wakati wa hafla hiyo.

Mtaalamu huyo wa Masoko ya Fedha Kimataifa kutoka Absa pia alizipongeza taasisi za udhibiti, zikiwemo Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa mchango wao endelevu katika kujenga imani ya washiriki wa soko na kuunga mkono ukuaji endelevu wa sekta ya fedha.

Tukio hilo pia lilinufaika na ushiriki wa wataalamu wa Absa kutoka masoko mbalimbali barani Afrika, waliohudhuria ana kwa ana na kwa njia ya mtandao, jambo lililoonyesha kuongezeka kwa muunganiko wa masoko ya fedha barani humo pamoja na umuhimu wa kubadilishana maarifa.

Wakati wa semina hiyo, washiriki walipatiwa mawasilisho kuhusu mwenendo wa uchumi mpana unaoathiri Tanzania na dunia kwa ujumla, mikakati ya kusimamia hatari zinazotokana na mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji fedha za kigeni na viwango vya riba, pamoja na suluhisho za uwekezaji zinazolenga kuongeza faida ya uwekezaji huku zikizingatia viwango vya hatari vinavyokubalika kwa taasisi husika.

Kwa mujibu wa Absa, kikao hicho ni sehemu ya dhamira pana ya benki hiyo ya kuwawezesha wawekezaji kupitia taarifa na uchambuzi wa masoko unaoweza kutumika moja kwa moja katika kufanya maamuzi, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu na wateja wake wa taasisi.

Kikiwa kimeandaliwa chini ya Lengo la Benki ya Absa la “Kuiwezesha Afrika ya Kesho, pamoja... Hatua moja baada ya nyingine,” semina hiyo ililenga kuwapatia wawekezaji maarifa na nyenzo zinazohitajika kufanya maamuzi sahihi katika mazingira ya soko yanayobadilika na kutumia fursa mpya zinazojitokeza ndani na nje ya Tanzania.

Mmoja wa washiriki katika semina hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Ushauri wa Kifedha ya Exodus Advisory, Bw. Ramadhan Kagwandi alishauri kutokana na Athari za kiuchumi zinazotokana na majanga ya kidunia hususani suala la kupanda kwa bei ya mafuta akisema juhudi hazina budi kufanyika katika kufanya uwekezaji mkubwa katika matumizi ya nishati mbadala wa mafuta, hususani matumizi ya gesi.

“La pili serikali inapaswa kuangalia namna nchi yetu inaweza kuwa na akiba ya kutosha ya mafuta endapo tutahitai kuendelea kutumia nishati hiyo, lakini lingine likiwa ni suluhisho la muda mrefu kama nchi ni kuwa na Uchumi unaojitegemea, na hili naona serikali imeshalifanyia kazi katika Bajeti ya 2026/2026 ikionesha kuwa asilimia karibu 75 ya bajeti inategemea vyanzo vya ndani,” alisemwa Bw. Kagwandi.

Kwa upande wake mshiriki mwingine, Bw. Beatus Mlingi, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Diamond Global Securities alitoa shukurani kwa Benki ya Absa kwa kuwa na ubunifu katika kuandaa semina hiyo, kwani imewasaidia kupata masuluhisho mengine ya jinsi ya kuweza kufanya biashara zao kwa ufanisi licha changamoto mbalimbali zinazojitokeza.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Masoko ya Fedha za Kigeni wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Irene Rwegalulira (kulia), na Mtaalamu Mwandamizi wa Masuala ya Biashara kutoka Absa Group, Bw. Gerald Nana (kushoto) wakizungumza na baadhi ya washiriki kutoka taasisi kubwa za uwekezaji wakati ya warsha ya siku moja iliyoandaliwa na benki hiyo ili kutoa mwelekeo wa kiuchumi wa ndani na nchi nyingine mbalimbali duniani, iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.



Mkurugenzi wa Kitengo cha Masoko ya Fedha za Kigeni wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Irene Rwegalulira akizungumza na baadhi ya washiriki kutoka taasisi kubwa za uwekezaji, wakati akifungua rasmi warsha ya siku moja iliyoandaliwa na benki hiyo ili kutoa mwelekeo wa kiuchumi wa ndani na nchi nyingine mbalimbali duniani, iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Mtaalamu Mwandamizi wa Masuala ya Biashara kutoka Absa Group, Bw. Kabelo Bogopa akizungumza na baadhi ya washiriki kutoka taasisi kubwa za uwekezaji wakati ya warsha ya siku moja iliyoandaliwa na benki hiyo ili kutoa mwelekeo wa kiuchumi wa ndani na nchi nyingine mbalimbali duniani, iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.

 Mkuu wa Masoko ya Fedha za Kigeni wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Elisia Temu (kulia) akizungumza na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Exodus Advisory, Bw. Ramadhani Kagwandi wakati ya warsha ya siku moja iliyoandaliwa na benki hiyo ili kutoa mwelekeo wa kiuchumi wa ndani na nchi nyingine mbalimbali duniani, iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.




Mkurugenzi wa Kitengo cha Masoko ya Fedha za Kigeni wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Irene Rwegalulira (katikati) akipiga picha ya pamoja na washiriki kutoka taasisi kubwa za uwekezaji na wafanyakazi kutoka benki hiyo hiyo, wakati ya warsha ya siku moja iliyoandaliwa na Benki ya Absa, ili kutoa mwelekeo wa kiuchumi wa ndani na nchi nyingine mbalimbali duniani, iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...