Na Janeth Raphael MichuziTv - Bungeni Dodoma

Serikali imeeleza kuwa inaendelea kutekeleza mkakati wa muda mrefu wa kuwawezesha vijana, wakiwemo wenye mahitaji maalum, kupitia vikundi vilivyosajiliwa ili kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.

Kauli hiyo imetolewa bungeni na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma kwa niaba ya

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Latifa Khamis Juwakali, aliyetaka kufahamu mipango ya Serikali katika kuwawezesha vijana wenye vikundi vilivyosajiliwa pamoja na wenye mahitaji maalum.

Waziri huyo amesema kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi yanayolenga kuongeza fursa za ajira, ujasiriamali na maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa vijana kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji.

Amefafanua kuwa uwezeshaji huo unajumuisha utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, pamoja na Programu ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi inayotekelezwa kupitia shilingi bilioni 200 zilizotolewa kufuatia ahadi ya Rais.

Aidha, Serikali inaendelea kutoa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, hatua inayolenga kusaidia vikundi vya vijana kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji mali.

Katika kuimarisha ushiriki wa makundi maalum katika uchumi, Serikali pia inaendelea kutekeleza utaratibu wa kutenga asilimia 30 ya zabuni za umma kwa vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum ili kuwapa fursa zaidi za kushiriki katika shughuli za biashara na utoaji wa huduma.

Sambamba na hilo, Serikali imeendelea kuunganisha vikundi vya vijana na taasisi za kifedha pamoja na kuimarisha mifumo ya uratibu na utoaji wa taarifa, hatua zinazolenga kuongeza upatikanaji wa mitaji, fursa za biashara na ajira.

Hatua hizo zinaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha vijana na watu wenye mahitaji maalum wanapata fursa stahiki za kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...