Na Janeth Raphael-MichuziTv


Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limeahidi kuchangia fedha kwa ajili ya kuimarisha huduma za upandikizaji figo na uroto (selimundu) katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha huduma za afya nchini kuelekea maadhimisho ya miaka 10 ya hospitali hiyo yanayotarajiwa kufanyika Julai 15, 2026.

Akizungumza wakati wa ziara ya wahariri wa vyombo mbalimballi vya habari nchini katika hospitali hiyo jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Deodatus Balile, amesema mchango huo unalenga kusaidia wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu ya kibingwa yanayotolewa na hospitali hiyo.

Balile amesema huduma za kibingwa zinazopatikana BMH zimekuwa mkombozi kwa Watanzania wengi kutokana na ubora wake na gharama nafuu ikilinganishwa na matibabu yanayopatikana nje ya nchi.

“Hakuna mtu ambaye hapendi kupata huduma bora kwa gharama nafuu. Sisi kama wahariri tumeona ni muhimu kuunga mkono juhudi hizi kwa kuchangia ili kuwasaidia wale wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu,” amessema Balile.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dkt. Abdalla Baja, amesema hospitali hiyo imeendelea kupanua wigo wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, ikiwa na madaktari bingwa bobezi 18 pamoja na madaktari bingwa 20 wanaotoa huduma mbalimbali za matibabu ya hali ya juu.

Amesema mbali na huduma za upandikizaji figo na uroto, hospitali hiyo imefikia hatua ya kutoa huduma za upandikizaji wa uume kwa wagonjwa wenye changamoto zinazohitaji tiba hiyo maalumu.

Dkt. Baja aliongeza kuwa BMH imeandika historia kwa kuwa hospitali ya kwanza Afrika Mashariki kufanya upandikizaji wa uroto (selimundu), hatua ambayo imeifanya kuwa kituo muhimu cha rufaa kwa wagonjwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kati.

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu, Dkt. Happiness Joseph Igogo, alisema hospitali hiyo imejipanga kuongeza idadi ya wagonjwa wanaopatiwa huduma za upandikizaji wa uroto kutoka wagonjwa 10 hadi 20 kwa mwaka.

Amesema mafanikio ya huduma hiyo yamechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa wa selimundu na kutoa matumaini mapya kwa wagonjwa wengi.

Kwa upande wake, Meneja wa Mkoa wa Dodoma wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Irene Kataraihya, alisema taasisi hiyo imejipanga kushiriki kikamilifu katika mfuko maalumu wa kusaidia huduma hizo muhimu ili kuendelea kuokoa maisha ya Watanzania.

Akizungumzia huduma za figo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani na Figo, Dk. Ayubu Masamba, amesema huduma za upandikizaji figo zinazotolewa BMH zimepunguza kwa kiwango kikubwa idadi ya wagonjwa waliokuwa wakisafiri nje ya nchi kutafuta matibabu hayo.

Amesema hatua hiyo imechangia kupunguza gharama kubwa za matibabu kwa wagonjwa na familia zao huku ikiimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa ndani ya Tanzania.

Maadhimisho ya miaka 10 ya Hospitali ya Benjamin Mkapa yanatarajiwa kuwa fursa ya kuonesha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utoaji wa huduma za afya za kibingwa na ubingwa bobezi, huku hospitali hiyo ikiendelea kuwa kinara wa huduma za kisasa za matibabu nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...