Chuo cha Bahari Dar es Salaam kimewahimiza vijana na wanawake kujiunga na masomo ya fani za bahari, kikieleza kuwa sekta hiyo ina fursa kubwa za ajira na maendeleo kutokana na mahitaji ya wataalamu wenye ujuzi katika shughuli za baharini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Juni 23, 2026, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Makamu Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam anayeshughulikia Fedha, Mipango na Utawala, Prof. Lucas Mwisilla, amesema ushiriki wa chuo hicho katika maonyesho hayo umelenga kusogeza huduma karibu na wananchi, ikiwemo kutoa taarifa kuhusu programu za mafunzo, ushauri elekezi na shughuli za utafiti wa bahari.

Amesema kupitia maonyesho hayo, jumla ya wananchi 250 wamefika katika banda la chuo hicho na kupata huduma mbalimbali, wakiwemo wanafunzi, viongozi wa taasisi za serikali na binafsi pamoja na wadau wanaohusika na shughuli za baharini.

Prof. Mwisilla amesema Chuo cha Bahari Dar es Salaam kinaendelea kutoa mafunzo yenye kuendana na mahitaji ya soko la ajira, ambapo mwaka uliopita zaidi ya wahitimu 2,000 walimaliza masomo yao na kupata ajira katika taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi.

Amesema hali hiyo inaonesha kuwa kozi zinazotolewa na chuo hicho zina nafasi kubwa katika kuwajengea vijana uwezo wa kupata ajira na kujiajiri katika sekta ya bahari.

“Wazazi na walezi wanapaswa kuwahamasisha wanafunzi kujiunga na chuo hiki kwa kuchagua kozi bora zenye uhitaji mkubwa katika soko la ajira ili waweze kupata fursa nzuri baada ya kuhitimu.”

Aidha, amesema mwamko wa wanawake kujiunga na fani za bahari umeongezeka ukilinganisha na miaka ya nyuma, ambapo sasa baadhi yao wamepata ujuzi na wameajiriwa katika shughuli mbalimbali ikiwemo kufanya kazi kwenye meli.

Ametumia fursa hiyo kuwakaribisha zaidi wasichana na wanawake kuingia katika tasnia ya bahari, akisema sekta hiyo ina nafasi kubwa ya ajira na inahitaji ushiriki wa wataalamu kutoka makundi mbalimbali.

Amesisitiza kuwa chuo hicho kitaendelea kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali kuhakikisha kinatoa wataalamu wenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya sekta ya bahari nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...