-Zoezi la Uokoaji Kigoma Laonesha Uwekezaji wa Serikali Katika Usalama Majini
Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Rashid Chuachua, amesema kuwa usalama wa mabaharia na vyombo vya usafiri katika Ziwa Tanganyika ni jambo la msingi linalopaswa kupewa kipaumbele ili ziwa hilo liendelee kuwa nguzo muhimu ya uzalishaji na maendeleo ya uchumi wa Mkoa wa Kigoma na Taifa kwa ujumla.
Chuachua alitoa kauli hiyo wakati wa zoezi la majaribio ya utafutaji na uokoaji lililoshirikisha vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na Boti ya Utafutaji na Uokoaji ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), lililofanyika katika Bandari ya Kibilizi mkoani Kigoma.
Alisema kuwa kuimarishwa kwa mifumo ya uokoaji na usalama majini kutasaidia kupunguza madhara yanayotokana na ajali za vyombo vya majini, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza ukaguzi wa mara kwa mara wa vyombo hivyo ili kuzuia majanga yanayosababishwa na makosa ya kibinadamu.
“Ziwa Tanganyika ni rasilimali muhimu ya kiuchumi. Ili liendelee kutoa mchango wake kikamilifu, ni lazima tuhakikishe mabaharia na vyombo vya usafiri vinakuwa salama wakati wote,” alisema Chuachua.
Aidha, alisema maadhimisho ya Siku ya Mabaharia pamoja na maonesho ya zoezi la uokoaji yanaonesha dhamira ya Serikali katika kuwekeza kwenye vifaa na miundombinu ya kisasa ya uokoaji kwa lengo la kulinda maisha ya wananchi wanaotumia usafiri wa majini.
Chuachua pia aliwataka mabaharia na waendeshaji wa vyombo vya majini kuhakikisha wanazingatia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kabla ya kuanza safari zao ili kujiepusha na hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
“Ni muhimu kwa mabaharia kufuatilia utabiri wa hali ya hewa kabla ya kuanza safari. Hii itasaidia kulinda maisha yao pamoja na mizigo inayosafirishwa,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohamed Salum, alisema kuwa Boti ya Utafutaji na Uokoaji iliyowekwa katika Ziwa Tanganyika ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha usalama wa wananchi wanaosafiri kwa njia ya maji na kuhakikisha huduma za uokoaji zinapatikana kwa haraka pale majanga yanapotokea.
Alisema TASAC itaendelea kusimamia viwango vya usalama majini na kutoa huduma bora kwa mabaharia pamoja na wadau wengine wa sekta ya usafiri wa majini nchini.
“Tumeleta boti hii kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanaopata majanga majini wanapata msaada wa haraka.Pia tunaendelea kuhimiza mabaharia kutoa taarifa mapema wanapokumbana na changamoto ili hatua za uokoaji ziweze kuchukuliwa kwa wakati,” alisema Salum.
Zoezi hilo limeelezwa kuwa sehemu ya maandalizi ya kuimarisha uwezo wa kukabiliana na dharura majini na kuongeza uelewa wa wadau kuhusu umuhimu wa usalama katika sekta ya usafiri wa majini, hususan katika Ziwa Tanganyika ambalo ni moja ya njia muhimu za usafirishaji na biashara nchini.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Rashid Chuachua akizungumza wakati zoezi la jaribio la uokoaji lililofanyika katika Bandari ya Kibilizi ikiwa ni maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani yanayoendelea mkoani Kigoma.
Mkurugenzi Mkuu wa TASAC Mohamed Salum akitoa maelezo kuhusiana na zoezi la uokoaji lililofanyika katika Bandari ya Kibilizi katika maadhimisho ya 16 ya Siku Mabaharia Duniani yanayoendelea mkoani Kigoma.
Mkurugenzi wa Usalama wa Usafiri na Mazingira wa Wizara ya Uchukuzi Stella Katondo akizungumza kuhusiana na serikali ilivyowekeza katika uokoaji katika majanga ya usafiri wa majini kwenye maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani yanayoendelea mkoani Kigoma.
Baadhi ya matukio ya jaribio la uokoaji ya mmoja wa afisa aliyejirusha ziwani ili kupata msaada wa kuokolewa.




.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...