Na Janeth Raphael MichuziTv
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amewataka watumishi wa Wizara ya Madini na taasisi zake kushiriki kikamilifu katika shughuli za michezo na mazoezi ya mwili, akieleza kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kuimarisha afya ya akili, kujenga mshikamano mahali pa kazi na kuongeza ufanisi wa utendaji.
Akizungumza katika Bonanza la Michezo lililowakutanisha watumishi wa Wizara hiyo pamoja na Tasisi zilizo chini yake, Dkt. Kiruswa amesema michezo ina mchango mkubwa katika kuboresha afya za watumishi kwa kuwasaidia kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza na kuongeza ustawi wao wa kimwili na kiakili, Amesisitiza kuwa mazoezi ya mara kwa mara ni msingi wa maisha yenye afya na tija kazini.
Aidha, amesema michezo si chanzo cha burudani pekee bali pia ni fursa ya ajira na kuongeza kipato kupitia vipaji mbalimbali vinavyoweza kuibuliwa na kuendelezwa. Kwa mujibu wake, watumishi wanapaswa kuendeleza utamaduni wa kushiriki michezo ili kujenga afya bora, furaha na mahusiano mazuri katika mazingira ya kazi.
Bonanza hilo limewakutanisha watumishi wa Wizara ya Madini pamoja na taasisi zake zote katika utaratibu wa kawaida wa kukutana kila robo mwaka kwa lengo la kuimarisha ushirikiano, mshikamano na kufahamiana zaidi. Washiriki walipata nafasi ya kushiriki michezo mbalimbali ikiwemo jogging, mpira wa miguu, mpira wa pete, basketball, kuvuta kamba, riadha na michezo ya burudani iliyovutia ushiriki mkubwa wa watumishi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Yahya Samamba, amesema bonanza hilo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya viongozi wa Wizara ya kuhakikisha watumishi wanapata fursa za kufanya mazoezi na kuimarisha afya zao. Amebainisha kuwa ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza katika jamii linaifanya michezo kuwa moja ya njia muhimu za kinga na uhamasishaji wa maisha yenye afya.
Katika bonanza hilo, washindi wa michezo mbalimbali walitunukiwa medali na zawadi, huku wanamichezo waliowakilisha Wizara katika Mashindano ya Mei Mosi wakikabidhi vikombe viwili walivyovishinda katika mbio na mchezo wa pool table. Bonanza hilo limeelezwa kuwa hatua muhimu ya kuimarisha mahusiano, umoja na ari ya kazi miongoni mwa watumishi wa sekta ya madini, jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi wa utendaji na mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa nchi.


.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...