WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imejipanga kuanza ujenzi wa barabara ya Mafinga–Mgololo kwa kiwango cha lami katika mwaka wa fedha 2026/2027 huku ikiendelea kutekeleza miradi ya kuimarisha miundombinu ya umeme ili kuondoa changamoto ya kukatika kwa umeme katika Wilaya ya Mufindi.
Amesema hayo jana Jumamosi (Juni 6, 2026) alipokuwa akizungumza na kusikiliza kero za wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga mkoani Iringa.
Dkt. Mwigulu alisema barabara ya Mafinga–Mgololo ni miongoni mwa miradi ambayo utekelezaji wake ulipungua kasi kutokana na Serikali kuelekeza nguvu katika kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Reli ya Kisasa (SGR) na Daraja la Kigongo–Busisi.
“Nilikuwepo pale pale kwenye chungu, najua kona kona zile, najua ule ukoko utatoka wapi, fedha zije na barabara hii ianze kujengwa. Nitaisimamia na nitaifuatilia kwa sababu inaungana na ahadi za Mheshimiwa Rais na ahadi za Serikali kwa wananchi,” alisema.
Alisema Serikali imeanza utekelezaji wa mpango wa kufufua miradi ambayo mikataba yake ilishasainiwa pamoja na ile ambayo wakandarasi walikuwa bado hawajapewa malipo ya awali ili waweze kuingia maeneo ya kazi.
Kuhusu huduma ya maji, Dkt. Mwigulu alisema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi wa maji wa miji 28 ambao unalenga kuongeza upatikanaji wa maji katika Mji wa Mafinga na maeneo ya jirani. Alisema mradi huo ni miongoni mwa miradi ambayo awali ilikumbwa na changamoto za upatikanaji wa fedha baada ya kusainiwa kabla ya fedha kupatikana, lakini sasa Serikali imeweka utaratibu wa kuhakikisha fedha za miradi ya maji zinapelekwa moja kwa moja kwenye mifuko ya maji ili kuharakisha utekelezaji wake.
“Maji ni jambo la lazima, maji ni maisha. Mradi huu ni miongoni mwa miradi nitakayofuatilia kwa karibu ili ukamilike na wananchi wa Mafinga wapate huduma ya maji ya uhakika,” alisema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba alisema Serikali imetenga shilingi bilioni 3.9 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya umeme katika Wilaya ya Mufindi ikiwemo kutenganisha laini zinazohudumia viwanda na zile zinazohudumia matumizi ya majumbani.
Alisema Serikali pia inaendelea na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme katika eneo la Kisada pamoja na kuimarisha mtandao wa usambazaji wa umeme ili kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi na viwanda vya Mafinga.
Naye Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dkt. Jafar Seif alisema Serikali kupitia Mradi wa TACTIC inaendelea kuboresha miundombinu ya Halmashauri ya Mji wa Mafinga ikiwemo ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 11.8 pamoja na miundombinu ya soko la kisasa na stendi ya mabasi kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri, biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mji huo.
Alisema miradi hiyo itatekelezwa kupitia awamu ya tatu ya Mradi wa TACTIC na itanufaisha wananchi wa Mafinga kwa kuboresha mazingira ya biashara, usafiri na utoaji wa huduma za kijamii.
Dkt. Seif pia alisema Serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya katika Mji wa Mafinga ikiwemo kukamilisha mtambo wa kuzalisha hewa tiba (Oxygen Plant) ambao utahudumia Mkoa wa Iringa na maeneo mengine ya Nyanda za Juu Kusini. Alisema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha huduma za matibabu ya dharura na kuhakikisha upatikanaji wa hewa tiba katika hospitali za umma.
Awali, Mbunge wa Mafinga Mjini, Dickson Lutevele aliiomba Serikali kuharakisha utekelezaji wa mradi wa barabara ya Mafinga–Mgololo, kukamilisha mradi wa maji wa miji 28, kuimarisha huduma ya umeme pamoja na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya TACTIC kutokana na umuhimu wake katika kukuza shughuli za kiuchumi, viwanda na ustawi wa wananchi.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...