DODOMA Jiji wametwaa ubingwa wa jumla wa mashindano ya UMISSETA ngazi ya mkoa 2026 baada ya kuonyesha kiwango cha juu cha ushindani na kujikusanyia alama 255 zilizowahakikishia nafasi ya kwanza.
Ushindi huo umechangiwa na mwendelezo mzuri wa matokeo katika michezo mbalimbali ambapo wamenyakua vikombe 10, ikiwemo mpira wa kikapu (wavulana na wasichana), mpira wa mikono (wavulana na wasichana), mpira wa wavu wavulana, soka wasichana na kizazi kipya, huku wakimaliza nafasi ya pili katika mpira wa wavu wasichana.
Akizungumzia ushindi huo, Afisa Elimu Sekondari wa Jiji la Dodoma, Mwl. Daniel Mapilya, alisema mafanikio hayo yameambatana na uwakilishi mkubwa katika timu ya mkoa, ambapo kati ya wanafunzi 120 waliochaguliwa, 45 wametoka Jiji la Dodoma, hatua inayoonesha ubora wa maandalizi kuelekea mashindano ya kitaifa yatakayofanyika Iringa.
“Mafanikio hayo ni makubwa kwa jiji letu, na tunawapongeza walimu wa michezo, wakuu wa shule, maafisa utamaduni na michezo pamoja na maafisa elimu sekondari kwa mchango wao mkubwa uliowezesha ushindi huu kupatikana” alisema Mwl. Mapilya.
Nae, Afisa Michezo wa Jiji la Dodoma, Peter Ititi alisema mafanikio hayo yamechangiwa na ushirikiano mzuri kutoka kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma na Mbunge wa Jimbo la Mtumba ambao wamekuwa wakiwapa hamasa. Aliahidi kuwa wataendelea kufanya vizuri na kuongeza idadi ya makombe katika mashindano yajayo.
Kwa upande wake, Mchezaji wa Mpira wa Miguu wa Dodoma Jiji, Fortunata Mfaume aliyeteuliwa kuwakilisha timu katika mashindano ya kitaifa yatakayofanyika mkoani Iringa, alisema kuwa amejipanga kikamilifu kuhakikisha anatoa mchango wake kwa timu ya mkoa na kuiwezesha kufanya vizuri katika mashindano hayo.
Mafanikio ya Dodoma Jiji katika mashindano ya UMISETA ngazi ya mkoa 2026 yanadhihirisha maandalizi mazuri, mshikamano na ushindani wa hali ya juu. Timu hiyo sasa inaelekeza macho yake katika mashindano ya kitaifa, ikilenga kuendeleza rekodi yake ya ubabe kimichezo.


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...