Na Said Mwishehe,Michuzi TV


SEKRETARIATI ya Maadili ya Viongozi wa Umma imetoa rai kwa waandishi wa vyombo vya habari nchini kuendelea kutumia weledi wao kupitia kalamu na sauti zao kujenga Taifa moja lenye Viongozi na wananchi waadilifu.

Imetoa rai hiyo leo Juni 19,2026 Jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Maadili Jaji Sivangilwa Mwangesi wakati wa ufunguzi wa mkutano na wahariri wa vyombo vya habari nchini.

“Rai yangu kwenu, kuweni wazalendo kwa Taifa lenu. Endeleenii kutumia weledi wenu kupitia kalamu na sauti zenu kujenga Taifa moja lenye Viongozi na wananchi waadilifu. Maudhui ya habari mnazochapisha yaakisi umoja na mshikamano katika Taifa letu,”amesema Jaji Mwengesi.

Kuhusu lengo la mkutano huo amesema ni kuwajumuisha pamoja kuwa na sauti moja katika kukuza uadilifu miongoni mwa Viongozi wa Umma nchini huku akisisitiza ikumbukwe uadilifu wa viongozi wa umma una manufaa makubwa kwa vizazi vilivyopo na vijavyo katika Taifa letu.

Amefafanua Taifa lenye viongozi waadilifu, rasilimali zake zinanufaisha jamii nzima wakati kinyume chake rasilimali za nchi zinakuwa mikononi mwa kundi la watu wachache. “Hali hii husababisha manunguniko, upendeleo na mgawanyo wa rasilimali usio zingatia mizania ya usawa. “

Amewaomba Wahariri wa vyombo vya habari nchini kuendelea kushirikiana na Sekretarieti ya Maadili kwa lengo la kujenga Taifa lenye viongozi waadilifu na hivyo itapunguzq minong’ono na manung’uniko dhidi ya Viongozi wa Umma. “Wananchi wataipenda Serikali yao na amani itatamalaki.”

Amesisitiza kwa kufanya hivyo uadilifu miongoni mwa Viongozi wa Umma nchini utaongezeka, Taifa litakuwa na jamii inayozingatia misingi ya maadili na uwajibikaji katika sekta ya umma utaongezeka.

Aidha, amesema minong’ono na malalamiko dhidi ya viongozi wa umma na Serikali kwa ujumla itapungua. Raslimali za umma zitawanufaisha wananchi wote na Taifa letu litakuwa mfano wa kuigwa. Kazi hii iko mikononi mwetu

Ametumia nafasi hiyo kuvipongeza vyombo vya habari nchini hasa Wahariri kwa kutumia weledi na maadili ya kazi zao kukuza maadili na kudumisha amani, ikizingatiwa kuwa pamoja na uwepo wa utandawazi, maadili ya Mtanzania yameendelea kulindwa.

Pamoja na hayo amesema uhusiano kati ya taasisi hiyo na vyombo vya habari nchini unazidi kuimarika siku hadi siku. Vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele na msaada mkubwa katika kuimarisha uadilifu miongoni mwa Viongozi wa Umma siku hadi siku kwa kuchapisha baadhi ya habari zinazotusaidia kujua changamoto mbalimbali za kimaadili na tunazifanyia kazi.

“Kutokana na ushirikiano huu, katika mwaka huu wa fedha wa 2025/26 unaoelekea ukingoni, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imefanya ziara katika Kanda zake nane kuongea na Wahariri wa Kanda husika kuhusu umuhimu wa ushirikiano wa pande hizi mbili katika kukuza Maadili ya Viongozi wa Umma kwa maendeleo ya Taifa letu.”

Jaji Mwangesi ameviomba vyombo vya habari visirudi nyuma katika kuibua mijadala chanya ya kukuza na kuimarisha maadili nchini. “Ikumbukwe Wahariri wa vyombo vya habari na wanahabari kwa ujumla ni wadau wetu muhimu sana kwasababu mnatumia weledi wenu kukusanya, kuchakata na kusambaza taarifa haraka na kuishawishi jamii kufikia lengo fulani.”

Kuhusu Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilianzishwa kufuatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, hususan Ibara ya 132. Ibara hiyo iliweka msingi wa kisheria wa kuanzishwa kwa mfumo wa kusimamia maadili ya Viongozi wa Umma nchini.

Kutokana na Ibara hiyo, ilitungwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Na. 13 ya mwaka 1995.Sheria hiyo ndiyo iliyoanzisha rasmi mfumo wa maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na kuunda Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kama chombo cha kusimamia utekelezaji wake.

Katika ngazi ya utekelezaji, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inasimamia utekelezaji wa sheria hiyo. Ikumbukwe kuwa Taasisi hii peke yake haiwezi kufikia lengo bila kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Wahariri.

Kupitia ofisi hiyo, zikiwemo Ofisi zetu za Kanda, tuna jukumu la kuhakikisha utoaji wa elimu ya maadili unafanyika kwa weledi mkubwa ili kuongeza uelewa kwa jamii yetu kwenye mambo yanayohusiana na maadili ya Viongozi wa Umma.

Elimu hiyo imekuwa ikitolewa kwa njia mbalimbali hususan kupitia vyombo vya habari, semina, maonesho, kongamano na mikutano ya hadhara. Kazi hii tutaendelea nayo kwa kushirikiana na vyombo vya habari vilivyoko nchini kwa kuongeza ubunifu na mbinu mpya kulingana na hadhira tunayokutana nayo.













Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...