📍SONGWE

Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi imekagua na kupitia Mpango wa Ufungaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Shanta (New Luika Gold Mine) uliopo mkoani Songwe ili kuhakikisha mpango huo unazingatia matakwa ya Sheria ya Madini, Sura ya 123, pamoja na Kanuni za Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira za mwaka 2010.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi, Mhandisi Hamisi Kamando, amesema mapitio hayo yanalenga kuhakikisha mgodi una mpango madhubuti wa kurejesha mazingira katika hali salama baada ya shughuli za uchimbaji kukamilika, sambamba na kulinda afya na usalama wa wananchi wanaouzunguka mgodi huo.

Amesema kwa mujibu wa Sheria ya Madini na Kanuni ya 206 ya Kanuni za Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira za mwaka 2010, migodi yote ya kati na mikubwa inatakiwa kuandaa na kuwasilisha mipango ya ufungaji migodi kwa Mkaguzi Mkuu wa Migodi kwa ajili ya mapitio ya kitaalam kabla ya kuidhinishwa na Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi.

Mhandisi Kamando amefafanua kuwa jukumu la Kamati hiyo ni kupitia mipango ya ufungaji migodi na kutoa ushauri wa kitaalam ili kuhakikisha migodi inafungwa kwa kuzingatia viwango vya mazingira, usalama na afya, na siyo kusitisha shughuli za uzalishaji kabla ya migodi kumaliza rasilimali zake.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Shanta (New Luika Gold Mine), Mhandisi Exupery Lyimo, amesema mgodi huo unaendelea kutekeleza viwango vya usalama, afya na utunzaji wa mazingira na upo tayari kutekeleza maelekezo yote yatakayotolewa na Kamati ili kuboresha mpango wake wa ufungaji.

Kikao hicho kimewakutanisha wataalam kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Madini, Wizara ya Maji, Wizara ya Maliasili na Utalii, Tume ya Matumizi Endelevu ya Ardhi, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Tume ya Madini pamoja na viongozi wa Serikali wa ngazi ya wilaya.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...