Na Seif Mangwangi, Michuzi TV, Arusha,
MAHAKAMA ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu imesema Tanzania imekuwa ikikiuka baadhi ya haki za msingi za binadamu kwa kuendelea kutumia adhabu ya kifo ya lazima na utekelezaji wake kwa njia ya kunyongwa.
Hayo yameelezwa Juni5, 2026 Jijini Arusha na majaji wa Mahakama ya Haki za Binaadam na Watu, (AfCPHR), wakiongozwa na Rais wa Mahakama hiyo Jaji Blaise Tchikaya walipokuwa wakisoma hukumu ya kesi nne zilizowasilishwa mahakama hapo ikiwemo shauri lililofunguliwa na wafungwa watatu waliohukumiwa kifo kwa kosa la mauaji.
Aidha Mahakama hiyo imewamuru waombaji watatu katika shauri hilo kulipwa fidia ya Shilingi 300,000 kila mmoja kwa madhara ya kimaadili yaliyotokana na ukiukwaji wa haki zao.
Uamuzi huo umeonyesha Serikali ya Tanzania ilishindwa kutekeleza wajibu wake wa kulinda na kuheshimu haki za binadamu katika eneo la utoaji na utekelezaji wa adhabu ya kifo kwa mujibu wa viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.
Hukumu hiyo ilitolewa mjini Arusha katika kesi iliyowahusisha Godfrey Gabinus Ndimba na wenzake wawili dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo waombaji hao walikuwa wamefungwa katika Gereza la Wilaya ya Lindi wakisubiri utekelezaji wa adhabu ya kifo baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la mauaji.
Katika maombi yao, waombaji hao walidai kuwa haki zao zilikiukwa wakati wa uchunguzi, usikilizwaji na utoaji wa hukumu katika mahakama za ndani. Walieleza kuwa kulikuwa na kasoro mbalimbali zilizowaathiri katika kupata haki stahiki.
Mahakama hiyo ya Afrika ilibaini kuwa Serikali ya Tanzania haikuwasilisha majibu yoyote katika shauri hilo licha ya kupewa taarifa zote muhimu na muda wa kutosha kufanya hivyo na kutokana na hali hiyo, Mahakama iliamua kutoa hukumu kwa kutokuwepo kwa upande wa Serikali.
Kabla ya kuamua shauri hilo, Mahakama ilijiridhisha kuwa ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kubaini kuwa madai yaliyowasilishwa yalihusu haki zinazolindwa chini ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu pamoja na mikataba mingine ya kimataifa iliyoridhiwa na Tanzania.
Mahakama pia ilikubaliana kuwa waombaji walikuwa wametumia njia zote za ndani za kutafuta haki, ikiwemo kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania kabla ya kufikisha shauri lao katika Mahakama ya Afrika.
Katika uchambuzi wa madai ya ukiukwaji wa haki ya kusikilizwa kwa haki, Mahakama ilibaini kuwa waombaji hawakuwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai yao kuhusu kutengenezwa kwa ushahidi, uwakilishi wa kisheria na mwenendo wa kesi zao. Kutokana na hali hiyo, madai hayo yalitupiliwa mbali.
Kadhalika, madai ya ukiukwaji wa haki ya usawa mbele ya sheria yalikataliwa baada ya Mahakama kubaini kuwa hayakuungwa mkono na ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa waombaji walitendewa tofauti au kunyimwa ulinzi sawa wa kisheria.
Hata hivyo, Mahakama ilikubaliana na hoja kwamba utoaji wa adhabu ya kifo kwa lazima bila kuzingatia mazingira ya kila mshtakiwa ni ukiukwaji wa haki ya kuishi inayolindwa chini ya Kifungu cha 4 cha Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu.
Mahakama pia ilieleza kuwa utekelezaji wa adhabu ya kifo kwa njia ya kunyongwa ni ukiukwaji wa haki ya utu wa binadamu na heshima ya mtu kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 5 cha Mkataba huo.
Kutokana na maamuzi hayo, Mahakama ilihitimisha kuwa Tanzania ilikiuka wajibu wake chini ya Kifungu cha 1 cha Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu. Hata hivyo, Mahakama ilikataa maombi ya kufutwa kwa hukumu za ndani na kuwaachia huru waombaji, huku ikisisitiza kuwa fidia ya Shilingi 300,000 kwa kila mmoja ilikuwa hatua stahiki ya kurekebisha madhara ya ukiukwaji wa haki zilizobainika.



.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...