Mfuko huo unasimamiwa na CORE Securities Limited na unalenga kupanua fursa za uwekezaji na maandalizi ya maisha ya baada ya kustaafu kwa Watanzania wa makundi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
Uzinduzi na utambulisho rasmi wa mfuko huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam, ukihudhuriwa na wadau wa sekta ya fedha, masoko ya mitaji, wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi, pamoja na wawakilishi wa vyombo vya habari.
Hafla hiyo iliongozwa na Mtaalamu Mbobevu wa Masoko ya Mitaji na Dhamana, Dkt. Ibrahimu Mwangalaba, huku Afisa Mtendaji Mkuu wa CORE Securities Limited, CPA George Fumbuka, akiwaongoza viongozi wengine wa kampuni hiyo kuelezea manufaa na fursa zinazotokana na mfuko huo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Mwangalaba aliipongeza CORE Securities Limited kwa kuanzisha mfuko huo, akieleza kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha ujumuishaji wa kifedha na kupanua wigo wa huduma za uwekezaji kwa wananchi wengi zaidi.
Alisema kwa muda mrefu mipango ya kustaafu nchini imekuwa ikihusishwa zaidi na watu wenye ajira rasmi ambao ni takribani asilimia chache zaidi ya wananchi wote, hali iliyosababisha sehemu kubwa ya wananchi, hususan walio katika sekta isiyo rasmi, kukosa fursa za maandalizi ya maisha ya baadaye.
“Kupitia FPRF, taifa linapata jukwaa jumuishi linalomwezesha kila Mtanzania — awe ameajiriwa rasmi, amejiajiri, mfanyabiashara au anayejishughulisha na shughuli za sekta isiyo rasmi — kuwekeza na kujiandaa kwa maisha ya baadaye kwa uhuru, unyumbufu na heshima,” alisema Dkt. Mwangalaba.
Aidha, aliwahimiza wananchi kujenga utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza kwa malengo ya muda mrefu, huku akisisitiza umuhimu wa kupata ushauri wa kitaalamu kabla ya kufanya maamuzi ya uwekezaji.
“Mipango ya kustaafu haipaswi kuonekana kama fursa ya watu wachache wenye ajira rasmi pekee. Kila Mtanzania anastahili kuwa na usalama na heshima ya kifedha baada ya miaka yake ya uzalishaji, na mfuko huu ni sehemu ya suluhisho la kufanikisha lengo hilo...nawapongeza sana CORE Securities kwa mpango huu” alisisitiza.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa CORE Securities Limited, CPA George Fumbuka, alisema FPRF imeundwa kuziba mapengo yaliyopo katika mifumo ya kawaida ya pensheni kwa kutoa chaguzi zenye unyumbufu zaidi katika uwekezaji na upatikanaji wa mafao.
“Ingawa mifuko ya hifadhi ya jamii kama NSSF na PSSSF inaendelea kuwa na mchango mkubwa katika ustawi wa wananchi, FPRF imeundwa kuikamilisha mifumo hiyo kwa kutoa fursa za ziada za uwekezaji kwa watu ambao awali hawakuwa na nafasi ya kushiriki,” alisema.
Alifafanua kuwa CMSA iliidhinisha mfuko huo tarehe 28 Aprili 2026 kwa mujibu wa Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana pamoja na Kanuni za Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja za mwaka 1997, huku NMB Bank PLC ikiidhinishwa kuwa Mdhamini na Mlezi wa mfuko huo.
Kwa mujibu wa CPA Fumbuka, mfuko huo umeidhinishwa kukusanya hadi shilingi bilioni 10 kupitia uuzaji wa vipande vya uwekezaji milioni 100, kila kimoja kikiwa na thamani ya shilingi 100.
Alisema muundo wa FPRF umeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji tofauti ya kifedha na viwango vya uvumilivu wa hatari za uwekezaji kwa makundi mbalimbali ya umri.
“Mahitaji ya kifedha ya kijana aliyeanza kazi ni tofauti na ya mtu anayekaribia kustaafu. Ndiyo maana tumeandaa mipango tofauti inayowawezesha wawekezaji kuchagua mkakati unaoendana na umri, kipato na matarajio yao ya muda mrefu,” alieleza.
Mfuko huo utakuwa na mipango mitatu ya uwekezaji ambayo ni Youngsters’ Plan kwa wawekezaji wenye umri chini ya miaka 35, Middle-Agers’ Plan kwa wenye umri kati ya miaka 35 na 50, na Seniors’ Plan kwa wawekezaji wenye umri zaidi ya miaka 50, ambao uwekezaji wake utazingatia zaidi dhamana za Serikali.
CPA Fumbuka alibainisha kuwa tofauti na mifuko mingi ya pensheni inayohitaji michango ya muda mrefu kabla ya mafao kupatikana, FPRF ina kipindi cha miaka mitano pekee ambapo baada ya hapo, mwekezaji ataweza kupata fedha zake kwa mkupuo, kwa malipo ya pensheni ya kawaida au kwa mchanganyiko wa njia hizo.
“Mahitaji ya kifedha ya watu hubadilika kadri muda unavyokwenda. Wapo wanaohitaji mapato ya kila mwezi baada ya kustaafu, na wapo wanaoweza kuhitaji sehemu ya akiba zao kwa ajili ya matibabu, familia au biashara. Mfuko huu unawapa uhuru wa kufanya maamuzi hayo kulingana na mahitaji yao,” alisema.
Aliongeza kuwa mwananchi anaweza kuanza uwekezaji kwa kiasi cha shilingi 10,000 tu, sawa na vipande 100 vya uwekezaji, na kuongeza uwekezaji wake taratibu kulingana na uwezo wake wa kifedha.
Mbali na hilo, mfuko huo unatoa faida ya ukwasi (liquidity), ambapo baada ya kipindi cha miaka mitano, wawekezaji wataweza kuuza vipande vyao kwa thamani halisi ya mali za mfuko (NAV), huku malipo yakifanyika ndani ya siku mbili za biashara.
Uwekezaji katika mfuko huo utafanyika kwa njia ya kielektroniki kupitia mfumo wa CORE Securities Limited, matawi maalumu ya NMB Bank PLC pamoja na mawakala walioidhinishwa na kuunganishwa na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa wa chama hicho, Bw. Nelson Mabula, alisema CWT imejiridhisha kuhusu usalama, uwazi na manufaa ya mfuko huo kwa wanachama wake.
“Kiwango cha chini cha kuanzia uwekezaji cha shilingi 10,000 kinawapa fursa wanachama wetu wengi kushiriki. Tunaamini huu ni uwekezaji wenye manufaa kwa walimu na wafanyakazi wengine, na kama taasisi tutahamasisha wanachama wetu kushiriki ili wawe sehemu ya fursa hii ya kujenga ustawi wao wa kifedha wa muda mrefu,” alisema.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya CORE Securities Limited, CPA George Fumbuka, (kushoto) akimkabidhi Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) Bw. Nelson Mabula (kulia) mfuko wenye nyaraka muhimu kuhusu Mfuko Mpya wa Uwekezaji wa kustaafu unaofahamika kama Foresight Private Retirement Fund (FPRF), ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa mfuko huo wakati wa hafla ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo. Anaeshuhudia katikati ni Mtaalamu Mbobevu wa Masoko ya Mitaji na Dhamana, Dkt. Ibrahimu Mwangalaba. Mfuko huo unasimamiwa na CORE Securities Limited na unalenga kupanua fursa za uwekezaji na maandalizi ya maisha ya baada ya kustaafu kwa Watanzania wa makundi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya CORE Securities Limited, CPA George Fumbuka, (kushoto) akimkabidhi Mtaalamu Mbobevu wa Masoko ya Mitaji na Dhamana, Dkt. Ibrahimu Mwangalaba (kulia) mfuko wenye nyaraka muhimu kuhusu Mfuko Mpya wa Uwekezaji wa kustaafu unaofahamika kama Foresight Private Retirement Fund (FPRF), ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa mfuko huo wakati wa hafla ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo. Mfuko huo unasimamiwa na CORE Securities Limited na unalenga kupanua fursa za uwekezaji na maandalizi ya maisha ya baada ya kustaafu kwa Watanzania wa makundi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya CORE Securities Limited, CPA George Fumbuka, (kulia) akimkabidhi Mwakilishi kutoka benki ya NMB Bw Avith Massawe (kushoto) mfuko wenye nyaraka muhimu kuhusu Mfuko Mpya wa Uwekezaji wa kustaafu unaofahamika kama Foresight Private Retirement Fund (FPRF), ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa mfuko huo wakati wa hafla ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo. Mfuko huo unasimamiwa na CORE Securities Limited na unalenga kupanua fursa za uwekezaji na maandalizi ya maisha ya baada ya kustaafu kwa Watanzania wa makundi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi huku benki ya NMB ikiwa Mdhamini na Mlezi wa mfuko huo.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya CORE Securities Limited, CPA George Fumbuka, (wa pili kushoto) sambamba na Mtaalamu Mbobevu wa Masoko ya Mitaji na Dhamana, Dkt. Ibrahimu Mwangalaba (wa pili kuli), Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) Bw. Nelson Mabula (kulia) na Mwakilishi kutoka benki ya NMB Bw Avith Massawe (kushoto) wakionesha nyaraka ya muongozo kuhusu Mfuko Mpya wa Uwekezaji wa kustaafu unaofahamika kama Foresight Private Retirement Fund (FPRF), ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa mfuko huo wakati wa hafla ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo. Mfuko huo unasimamiwa na CORE Securities Limited na unalenga kupanua fursa za uwekezaji na maandalizi ya maisha ya baada ya kustaafu kwa Watanzania wa makundi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi huku benki ya NMB ikiwa Mdhamini na Mlezi wa mfuko huo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Mwangalaba (pichani) aliipongeza CORE Securities Limited kwa kuanzisha mfuko huo, akieleza kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha ujumuishaji wa kifedha na kupanua wigo wa huduma za uwekezaji kwa wananchi wengi zaidi.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa CORE Securities Limited, CPA George Fumbuka (pichani) alisema FPRF imeundwa kuziba mapengo yaliyopo katika mifumo ya kawaida ya pensheni kwa kutoa chaguzi zenye unyumbufu zaidi katika uwekezaji na upatikanaji wa mafao.
Msimamizi wa Mfumo wa Teknolojia wa Mfuko Mpya wa Uwekezaji wa kustaafu unaofahamika kama Foresight Private Retirement Fund (FPRF), Bw Ibrahim Isack (pichani) akifafanua kuhusu uendeshwaji wa mfumo wa teknolojia wa mfuko huo wakati wa hafla hiyo.
Uzinduzi na utambulisho rasmi wa mfuko huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam, ukihudhuriwa na wadau wa sekta ya fedha, masoko ya mitaji, wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi, pamoja na wawakilishi wa vyombo vya habari.












Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...