Na Janeth Raphael MichuziTv - Bungeni Dodoma 

Serikali imechukua Hatua Kudhibiti Migogoro ya Wakulima na Wafugaji Mto Lukuledi Ndanda

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI imesema inatambua changamoto ya uvamizi wa wafugaji katika maeneo ya wakulima katika ushoroba wa Mto Lukuledi, Jimbo la Ndanda, hususan wakati wa ukame ambapo migogoro ya matumizi ya ardhi huongezeka.

Akijibu swali bungeni leo Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Dkt  Jafar Seif ameeleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kudhibiti hali hiyo ili kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa kati ya wakulima na wafugaji.

Serikali imeeleza kuwa moja ya hatua kubwa zilizochukuliwa ni pamoja na kupima na kutenga maeneo maalum ya malisho yenye ukubwa wa takribani hekta 129,489.48 katika vijiji 30 vya Mkoa wa Lindi, ikiwemo vijiji vilivyo karibu na bonde la Mto Lukuledi, Ndanda. Hatua hii inalenga kupunguza msongamano wa mifugo katika maeneo ya kilimo na kuzuia migogoro inayojitokeza mara kwa mara.

Aidha, Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa kuachana na ufugaji wa kuhamahama na badala yake kuelekea katika ufugaji wa kisasa unaozingatia tija na biashara. Elimu hiyo inalenga pia kubadilisha mtazamo kuhusu matumizi bora ya ardhi na uhifadhi wa mazingira.

Serikali imetoa wito kwa wafugaji kote nchini kuhakikisha wanazingatia mipango ya matumizi bora ya ardhi pamoja na kutumia kikamilifu maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho kwa kuyaendeleza kupitia kuondoa vichaka na kupanda malisho yanayoendana na ikolojia ya maeneo husika.

Kwa mujibu wa Serikali, utekelezaji wa mikakati hiyo utasaidia kuhakikisha upatikanaji wa malisho ya kutosha mwaka mzima, kupunguza migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji, na hatimaye kuimarisha amani na maendeleo endelevu katika maeneo ya vijijini.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...