Na Janeth Raphael MichuziTv - Bungeni Dodoma

Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Revocatus Chipando maarufu kama Baba Levo, ameibua mjadala bungeni jijini Dodoma baada ya kutoa maoni yanayogusa namna sera na elimu ya kijinsia zinavyotekelezwa nchini, akisisitiza haja ya kuangaliwa kwa usawa wa pande zote mbili za kijinsia bila kuacha kundi lolote nyuma.

Mbunge huyo amezungumza hayo wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa mwaka wa fedha 2026/27 ambapo ameseleza kuwa maendeleo ya jamii hayawezi kufanikiwa ipasavyo endapo yatabaki yakilenga upande mmoja tu wa jamii.

Katika mchango wake, Baba Levo ameeleza kuwa kumekuwa na mitazamo inayojikita zaidi katika kumuwezesha mwanamke, jambo ambalo kwa mujibu wake ni muhimu, lakini akasisitiza kuwa wanaume nao wanapaswa kuingizwa kikamilifu katika mipango ya elimu na uelimishaji kuhusu masuala ya kijinsia na maendeleo ya familia. 

Alisema kuwa jamii ni mchanganyiko wa wanaume na wanawake hivyo sera zinazohusu maendeleo zinapaswa kuzingatia uhalisia huo kwa usawa ili kuepusha migongano na hisia za upendeleo kwa upande mmoja.

Mbunge huyo pia amegusia changamoto zinazojitokeza ndani ya mahusiano na ndoa, akieleza kuwa baadhi ya migogoro ya kifamilia hutokana na kutoelewana, ukosefu wa uwazi na wakati mwingine madai yanayoibua hisia kali kati ya wanandoa.

 Alisisitiza kuwa mawasiliano ya kweli na uaminifu ni msingi muhimu wa kuimarisha familia, akibainisha kuwa endapo jamii itashindwa kushughulikia changamoto hizo kwa mtazamo mpana, migogoro itaendelea kuathiri ustawi wa familia na jamii kwa ujumla.

Baba Levo amesitiza pia umuhimu wa elimu ya ukatili wa kijinsia kutolewa kwa uwiano, akisema kuwa ingawa wanawake wanapaswa kuendelea kulindwa na kupewa uelewa zaidi kutokana na changamoto wanazokumbana nazo, pia kuna haja ya kuwajengea wanaume uelewa wa namna ya kushughulikia changamoto za kifamilia na kuepuka migogoro inayoweza kusababisha matatizo makubwa katika jamii. 

Aliongeza kuwa baadhi ya matukio ya kifamilia huweza kusababisha hisia kali na migogoro endapo hakuna ukweli na uwazi kati ya pande zinazohusika.

Kauli hizo zimeibua mjadala mpana miongoni mwa wabunge na wananchi, ambapo baadhi wameunga mkono wito wake wa kuangalia usawa wa kijinsia kwa pande zote, huku wengine wakisisitiza kuwa juhudi za sasa bado zinapaswa kuendelea zaidi katika kuwawezesha wanawake kutokana na historia ya changamoto walizopitia. 

Hata hivyo, mjadala huo unaendelea kuonesha umuhimu wa kuangalia upya namna sera na elimu ya kijinsia zinavyotekelezwa ili kuhakikisha zinagusa jamii kwa usawa bila kuacha kundi lolote nyuma.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...