-Ni baada ya kuahidiwa kulipwa deni la sh. milioni 181


MKAZI WA CHUNYA, Bi Agnes Obeid Ole amelia machozi ya furaha mbele ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba baada ya kusikilizwa kero yake na kutolewa uamuzi kwamba mdaiwa atafutwe na amlipe sh. milioni 181 anazozidai.

“Kamanda wa Polisi mtafute huyo bwana. Mahakama ilikwishatoa hukumu na ikampa mama ushindi. Asakwe popote alipo, arudishe vifaa na arudishe fedha za huyu mama,” amesema Waziri Mkuu na kuamsha shangwe kwa wananchi waliokuwepo.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Juni 6, 2026) wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya soko la Ifunda, wilayani Iringa, mkoani Iringa.

Akielezea kero yake, Bi. Agnes alisema kuwa kabla mumewe hajafariki, walikuwa wanachimba dhahabu kwenye mgodi wao huko Chunya lakini walimuomba rafiki yao, Bw. Lelevasi Fishulo mwenye mashine za kuchenjua washirikiane naye ili baadaye wagawane naye faida.

"Tulipata sh. milioni 362 lakini akasema amepata dharura na akaomba atulipe baadaye. Tukamkubalia. Mgao wetu ulikuwa sh. milioni 181 lakini siku ya kulipwa mume wangu akafariki, kwa hiyo nikaacha kufuatilia sababu ya maombolezo."

Bi. Agnes anasema baada ya mwaka mmoja kupita akamfuata kudai hela yake lakini hakumpa. "Nikaenda Serikali ya kijiji akaitwa kwa miezi mitatu hakutokea, nikaenda polisi akaitwa lakini ikapita miezi minne hakutokea ndipo nikaenda mahakamani kwa masuala ya mirathi," amesema.

Amesema alifungua kesi ya madai ya kudhulumiwa mali baada ya mumewe kufariki na mahakama ikampa haki ya kuwa msimamizi wa mirathi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwagiza Kaimu Meneja TANROADS Mkoa wa Iringa, Mhandisi Hosea Machaka atafute fedha sh. milioni 47 za kumlipa Bi. Subira Mdoka ambaye anadai fidia ya shamba alilotoa kupisha ujenzi wa uwanja wa ndega wa Nduli.

Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa TANROADS walifanya malipo ya fidia ya eneo lenye ekari 11 kwa Bw. Taaban ilhali eneo likiwa na mgogoro ambao ulikuwa umeshafikishwa mahakamani.

"Tafuteni akiba zenu mumlipe huyu Mama fedha yake kabla ya tarehe 30 Juni, 2026, kisha ninyi muendelee kumdai huyo bwana aliyewatapeli. Katibu Tawala wa Mkoa mtafuteni huyo bwana huko chuoni aelezwe haya maamuzi," amesema Waziri Mkuu.

Mhandisi Machaka alikiri kuwa walimlipa Bw. Taaban fedha hiyo wakati hukumu ya mahakama ilimpa ushindi Bi. Subira na wakawa wanamwambia asubiri fedha itakayorejeshwa na Bw. Taaban ndipo wamrejeshee.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...